Michezo

Ni masaibu tu kwa Shujaa duru ya saba Raga ya Dunia

April 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

LICHA ya kukaribisha wachezaji wazoefu Andrew Amonde, Augustine Lugonzo, Nelson Oyoo, Eden Agero, Daniel Sikuta, Jeffrey Oluoch na Oscar Dennis, Shujaa iliendelea kusalia ‘kibogoyo’ bila meno ya kung’ata wapinzani baada ya kupoteza mechi zake za Kundi B dhidi ya Fiji, New Zealand na Australia katika duru ya saba inayoendelea mjini Hong Kong.

Matumaini ya Kenya kujiokoa kutoka katika hatari ya kupoteza nafasi yake kwenye Raga ya Dunia yanazidi kudidimia zaidi baada ya kupepetwa na Fiji 22-5 Ijumaa na kuaibishwa na New Zealand 36-0 na Australia 28-12 Jumamosi.

Vichapo hivi vinaiteremsha Shujaa kupigania nafasi nane za mwisho kwenye ligi hii ya mataifa 15, ambayo yanakuwa na timu alikwa katika kila duru.

Shujaa iliingia duru ya Hong Kong ikishikilia nafasi ya 14 kwa alama 18 sawa na nambari 13 Wales, alama nne pekee kutoka nafasi ya 15 ambayo mshikilizi wa nafasi hiyo baada ya duru 10 kukamilika ataaga mashindano haya ya kifahari.

Wales na Japan zitakutana katika mojawapo ya mechi ya kutafuta nambari 9-16 baada ya kukosa kufuzu kushiriki robo-fainali kuu.

Kenya ya kocha Paul Murungha itamenyana na nambari 12 Canada, ambayo ina alama 35, katika mechi nyingine ya robo-fainali ya Challenge Trophy saa kumi na moja na dakika 36 asubuhi Jumapili.