• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
Jombi pabaya kudai mali aliyokopesha marehemu

Jombi pabaya kudai mali aliyokopesha marehemu

Na John Musyoki

MEKA, EMBU

KISANGA kilizuka katika boma moja hapa jamaa alipofurushwa mazishini kwa kutaka kubeba mali ya marehemu.

Inasemekana jamaa alikuwa mgeni katika kijiji hicho na wakazi walidhani alikuwa amehudhuria mazishi ya mwendazake.

Baada ya mwili kuzikwa jamaa alitaka afunguliwe nyumba ya marehemu achukue mali aliyokuwa amemkopesha.

“Naomba nifunguliwe nyumba ya marehemu nichukue mali yangu. Nilikuwa nimemkopesha bidhaa zangu na sasa nataka kuzibeba kwa sababu hakuwa amenilipa,” jamaa alisema.

Watu walipigwa na butwaa na kuanza kunong’onezana chini kwa chini.

“Kwanza huyu ni nani. Hatumjui wala hatujawahi kumuona hapa kijijini. Kwani marehemu alikuwa na madeni chungu nzima alikokuwa akiishi?” mama mmoja alisikika akishangaa.

Hata hivyo, licha ya jamaa kujaribu kujitetea juhudi zake ziligonga mwamba.

“Kuweni wapole. Nilimkopesha marehemu bidhaa zangu na hajawahi kulipa. Pia nilimpa mkopo wa pesa agharamie ujenzi wa nyumba hii yake. Sina mengi, nataka kubeba, meza, kabati na sofa. Kwa sasa mali ni yangu kwa sababu hakunilipa na siiachi,” jamaa aliambia watu.

Inasemekana watu walimrukia na kumsukuma kwa fujo wakitaka kumcharaza lakini jamaa akajinasua.

“Wewe ni tapeli. Kufumba na kufumbua macho, hatutaki kukuona hapa.

Hata kama marehemu alikuwa na deni lako unapaswa kudai kwa heshima. Hatukujui wala hatukutambui. Usilete kisirani chako hapa,” jamaa mmoja alisikika wakimwambia jamaa.

Jamaa kuona hivyo aliamua kuondoka bomani akihofia usalama wake. Hata hivyo haikujulikana ikiwa polo alikuwa akimdai marehemu.

 

You can share this post!

Kaunti za Pwani zatahadharisha wakazi kuhusu mafuriko yajayo

JAMVI: Kilele cha Ruto kumkaidi Uhuru

adminleo