Super Solico kutesa fainali za kitaifa Chapa Dimba na Safaricom
Na JOHN KIMWERE
KIKOSI cha wavulana wa Super Solico kimepania kutifua vumbi kali kwenye fainali za kitaifa kupigania taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Two mwaka huu zitakazofanyika Mwezi Juni katika uwanja wa Kinoru Stadium, mjini Meru.
Super Solico ilinyakua tiketi ya fainali hizo ilipoibuka mabingwa wa Mkoa wa Mashariki kwa kulaza Isiolo Young Stars mabao 5-4 baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika fainali iliyoandaliwa Kitui Show Ground mjini humo. Kwenye nusu fainali, Super Solico ya Mwingi iliikomoa Samba FC ya Marsabit mabao 3-2.
Super Solico ilitwaa taji badala ya Mwingi Junior Stars iliyokuwa mabingwa wa kipute mkoani huo msimu uliyopita.
”Nina imani vijana wangu wanao uwezo wa kufanya kweli kwenye ngarambe hiyo maana nazidi kufuatilia jinsi wapinzani wetu wanavyocheza katika fainali za maeneo yao,” kocha wake, Bernard Mudachi Kihima alisema na kuongeza kuwa wamepania kupiga kambi ya mwezi mmoja kabla ya kuelekea mjini Meru kushiriki michezo hiyo.
Pia anashukuru wote waliowaunga mkono kwenye juhudi zao ingawa baadhi yao hawakuwatarajia kikosi hicho kupiga hatua hiyo.
Anashukuru chipukizi hao kwa kazi njema waliofanya kwenye michuano ya msimu huu na kuwapiku wapinzani wao katika mkoa mzima. ”Hakika migarazano ya mwaka huu ilishuhudia ushindani mkali kuliko msimu uliyopita uliyopita na kuibuka mabingwa wa mkoa kamwe haikuwa mteremko,” alisema.
Kadhalika alikiri kwamba fainali za kitaifa zinatazamiwa kuzua msisimko wa kufa mtu kinyume na ilivyokuwa msimu uliyopita.
Kwenye mechi za mashindani Super Solico iliicharaza ITG mabao 2-0, kisha kubeba mabao 9-0 dhidi ya Down Town FC. Pia iliishinda Matrix FC mabao 2-1, kukomoa Tumaini FC magoli 4-2 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoshana nguvu bao 1-1, kabla ya kubamiza Utoo kwa mabao 2-0 katika fainali iliyowapa tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za Mkoa wa Mashariki.
Kocha huyo anasema eneo la Mwingi limefurika chipukizi wengi wenye talanta lakini mara nyingi hukosa kutambuliwa na kuyeyusha matumaini ya kuonyesha ujuzi wao katika kandanda. Super Solico inajumuisha chipukizi kama: Robert Ngusya, Samwel Muthui, Bonface London, Edward Jefa, Christopher Mziza, James Mutua, Ali Nasri (nahodha), Vincent Onyango, Dennis Malombe, Evans Ochieng, Evans Mutuse na Eric Zakayo.
Timu zingine ambazo tayari zimenasa tiketi ya fainali za kitaifa ni pamoja na St Marys Ndovea-wasichana (Eastern) Al Ahly na Kitale Queens wavulana na wasichana(Rift Valley), Lugari Blue Saints (wavulana) na Bishop Njenga Girls (Western) pia Manyatta Boys na Ndhiwa Queens(Nyanza).