Chepkoech awabwaga wapinzani kwenye IAAF World Indoor Tour
Na GEOFFREY ANENE
MKENYA Beatrice Chepkoech alitia kibindoni Sh2, 340,595 katika siku ya mwisho ya Riadha za IAAF World Indoor Tour zilizokamilika mjini Glasgow, Scotland, Februari 25, 2018.
Chepkoech alifahamu vyema kuwa ushindi utamweka juu ya jedwali la mbio za mita 1,500.
Akiwa na ufahamu huo, mkimbiaji huyu, ambaye ni gwiji wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, hakufanya masihara. Alifuata mwekaji kasi unyounyo katika mizunguko ya kwanza kabla ya kumpita na kufungua mwanya mkubwa kati yake na mpinzani wake wa karibu Muethiopia Axumawit Embaye.
Chepkoech alikamilisha mbio wa kwanza kwa dakika 4:02.21 na kujinyakua tuzo ya mshindi ya Sh305, 295 na kuongezwa Sh2, 035,300 kwa kushinda msimu.
Alimaliza msimu mbele ya Muethiopia Genzebe Dibaba (alama 20), Mjerumani Konstanze Klosterhalfen (14), Mmoroko Rababe Arafi (13) na Mkenya Winny Chebet (13).
Mbali na kupata ufanisi huo, Chepkoech pia anamiliki rekodi mpya ya Kenya ya mbio za ukumbini za mita 1,500 ya dakika 4:02.21 baada ya kufuta rekodi ya 4:02:23 aliyoweka mwaka 2017.
Mkenya Justus Soget alijishindia Sh305, 100 kwa kunyakua taji la Glasgow la mbio za mita 3,000 kwa dakika 7:39.09. Soget alimaliza msimu nyuma ya Waethiopia Yomif Kejelcha (alama 22) na Hagos Gebrehiwet (17), Mhispania Adel Mechaal (11) na Mkenya Edward Cheserek (10).
Mjini Glasgow, Soget alifuatwa kwa karibu na Muamerika Paul Chelimo (7:39.10), Kejelcha (7:39.36) na Mkenya Davis Kiplangat (7:40.12).
Wakenya Bethwell Birgen na Vincent Kibet walinyakua nafasi mbili za kwanza katika mbio za mita 1,500 mjini Glasgow kwa dakika 3:37.76 na 3:37.88 naye raia wa Australia, Ryan Gregson akafunga tatu-bora (3:38.00).
Mashindano ya IAAF World Indoor Tour yalianza Februari 3 mjini Karlsruhe mjini Ujerumani na kuzuru miji ya Dusseldorf nchini Ujerumani (Februari 6), Madrid nchini Uhispania (Februari 8), Boston nchini Marekani (Februari 10), Torun nchini Poland (Februari 15) kabla ya kufikia kilele mjini Glasgow (Februari 25).