MAPOZI: Kidum
NI mmojawapo wa wanamuziki wa kigeni wanaofanya vyema katika fani ya muziki nchini.
Kwa mashabiki zake anafahamika kama Kidum, lakini jina lake halisi ni Jean-Pierre Nimbona, msanii mzaliwa wa Burundi ambaye amejiundia jina sio tu kama mwanamuziki, bali pia utunzi na upigaji ngoma.
Mojawapo ya sababu ambazo zimemfanya kuendelea kung’aa kimuziki ni ushupavu wake katika utunzi ambapo anajumuisha wasanii wachache wanaotambulika kwa nyimbo zao zenye ujumbe na mdundo wa kuvutia huku mara nyingi nyimbo zake zikihusisha za kilimwengu na kiroho.
Baadhi ya nyimbo zake ni pamoja na ‘Nitafanya’, ‘Haturudi Nyuma’, ‘Mungu Anaweza’, ‘Kichuna’, ‘Pete’, ‘Mapenzi’, ‘Relax’, ‘Kimbia’ na ‘Mulika Mwizi’ miongoni mwa zingine.
Kazi hii nzuri imemfanya kutambuliwa katika baadhi ya tuzo za haiba ya juu sio tu Afrika Mashariki, bali barani kote huku akiwahi kupokea tuzo za Kora Awards.
Na katika harakati hizo amejiundia heshima kiasi cha wasanii wengi wanaofanya vyema katika eneo hili kutaka kushirikiana naye, na hata kutawazwa kama mjumbe wa amani kutokana na juhudi zake za kukuza matumaini na maridhiano eneo la Afrika Mashariki.
Albamu yake ya kwanza kwa jina Yaramenje aliyoizindua mwaka wa 2001 ndiyo iliyomthibitisha kama sauti ya amani katika eneo hili la Afrika.
Hii ilifuatiwa na albamu yake ya pili kwa jina Shamba, miaka miwili baadaye. Hakuonyesha ishara za kulegea kwani mwaka wa 2006 aliangusha albamu ya Ishano iliyojumuisha vibao vyake maarufu ikiwa ni pamoja na ‘Kichuna’.
Mwaka wa 2010 alizindua albamu yake Haturudi Nyuma iliyojumuisha vibao maarufu kama vile Mapenzi, Nitafanya na Haturudi Nyuma, na kwa mara ya kwanza kumshindia tuzo ya Kora Awards.
Mwaka wa 2012, alizindua albamu yake kwa jina Hali Na Mali iliyojumuisha vibao kama vile Mulika Mwizi, Kimbia, Enjoy na Hali Na Mali.
Kidum alijihusisha na muziki kwa mara ya kwanza mwaka wa 1984 akiwa na miaka kumi pekee ambapo alianza kama mcheza ngoma.
Miaka miwili baadaye alijiunga na bendi ya Imvumero Band ambapo alifanya kazi hapo kwa miaka sita.
Baadaye alijiunga na bendi ya Imboneza Band, iliyokuwa inamilikiwa na chama tawala nchini Burundi UPRONA ambapo aliichezea kati ya mwaka wa 1992 na 1993.
Kujihusisha kwake na bendi hizi kulimpa mfichuo na tajriba katika muziki ambapo mwaka wa 1994 alizindua bendi yake kwa jina Electric Power.
Hata hivyo, kutokana na vita vya kikabila nchini humo, bendi hiyo ilidumu kwa mwaka mmoja pekee.
Ni matatizo hayo ya kisiasa yaliyomsababisha mwaka wa 1995 kutoroka kutoka nchini mwake na kuhamia hapa Kenya ambapo alitarajia kuendeleza kipaji chake cha uimbaji.
Na haikuwa muda kabla ya kuanza kuonyesha kipaji chake kwani pindi baadaye alijiunga na bendi ya Hot Rod Band ambapo aliimba hapo hadi mwaka wa 2003.
Hii ilikuwa hadi alipoanzisha bendi yake ya Boda Boda Band mwaka wa 2004, ambayo anaiendesha hadi sasa.
Bendi yake imefanya shoo katika sehemu mbali mbali ulimwenguni ikiwa ni pamoja Mashariki ya Kati, Ulaya, Amerika na Amerika Kusini.
Sifa kuu ambayo imezidi kumtenganisha na wasanii wengine wa kawaida ni vipaji vyake tofauti katika usanii kama muimbaji, mpiga ngoma na mtunzi, huku uwezo wake wa kupitisha ujumbe kwa lugha tofauti ikiwa ni pamoja na Kiswahili, Kiingereza na Kihispania pia ukipanua himaya yake ya mashabiki na hivyo kumtambulisha zaidi.