OTEA MBALI: Manchester City waendea Tottenham Hotspur
Na MASHIRIKA
LONDON, UINGEREZA
TOTTENHAM Hotspur watakuwa leo Jumanne wenyeji wa Manchester City katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa robo-fainali ya kuwania ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Kwingineko, Liverpool wanatarajiwa kutamba dhidi ya FC Porto watakaokuwa wageni wao uwanjani Anfield. Liverpool waliwabandua Bayern Munich ya Ujerumani katika hatua ya 16-bora.
Miamba hao wa soka ya Uingereza walipokeza Porto kichapo cha 5-0 kwenye robo-fainali ya UEFA msimu jana.
Porto ambao kwa sasa wananolewa na kocha Sergio Coceicao, walifuzu kwa robo-fainali baada ya kuwabandua AS Roma ya Italia.
Kikosi hicho kinatazamiwa kutegemea pakubwa maarifa ya fowadi Moussa Marega ambaye amefunga mabao sita katika UEFA hadi kufikia sasa.
Mshindi wa mechi hizo za mikondo miwili atajikatia tiketi ya kuvaana ama na Barcelona au Manchester United kwenye nusu-fainali. Itakuwa ni mara ya pili kwa vijana wa kocha Mauricio Pochettino kusakata gozi katika uwanja wao wa nyumbani, Tottenham Hotspur Stadium.
Katika mchuano wao wa kwanza uwanjani humu, Tottenham walichuma nafuu kutokana na wingi wa mashabiki wao wa nyumbani na kuwapepeta Crystal Palace 2-0.
Ushindi huo uliowapaisha hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), ulikuwa wao wa kwanza kuvuna nyumbani tangu Februari.
Japo Tottenham wanapigiwa upatu wa kuyazima makali ya Manchester City, huenda hilo likawawia vigumu hasa ikizingatiwa ukatili ambao umedhihirishwa na masogora wa kocha Pep Guardiola katika michuano ya hivi karibuni. Man-City ambao wanapania kutia kapuni jumla ya mataji manne muhula, watajibwaga ugani wakijivunia ushindi wa 1-0 uliowashuhudia wakiwabandua Brighton kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA wikendi.
Awali, Man-City walikuwa wamewadhalilisha Schalke ya Ujerumani kwa kichapo cha 10-2 kwenye raundi ya 16-bora ya UEFA.
Borussia Dortmund yapigwa
Spurs kwa upande wao, walifuzu kwa robo-fainali za UEFA baada ya kuwaangusha Borussia Dortmund kutoka Ujerumani.
Pochettino anatarajiwa kumwajibisha mvamizi Fernando Llorente ambaye atashirikiana na Harry Kane kwenye safu ya mbele. Pigo kubwa kwa kikosi hicho ni ulazima wa kukosekana kwa beki Eric Dier, mvamizi Erik Lamela na difenda mzaliwa wa Ivory Coast, Serge Aurier.
Man-City watasubiri zaidi ripoti ya madaktari ili kufahamu hali ya jeraha la Sergio Aguero ambaye aliumia wakati wa mechi iliyowakutanisha na Fulham yapata wiki moja iliyopita.
Aguero hakuwa sehemu ya kikosi cha Man-City kilichowapepeta Brighton kwenye robo-fainali ya Kombe la FA wikendi jana.
Mchezaji mwingine ambaye huenda akakosa kuunga kikosi cha kwanza cha Man-City ni beki Kyle Walker ambaye kwa sasa anauguza jeraha la paja.
Beki Benjamin Mendy anatarajiwa kurejea ugani baada ya kupona jeraha. Hata hivyo, Fabian Delph na Oleksandr Zinchenko watasalia mkekani kwa muda zaidi kutokana na majeraha ya mguu na bega mtawalia.
Man-City wana fursa nyingine hii leo ya kuendeleza ubabe wao dhidi ya Spurs ambao waliwabamiza katika mchuano wa mkondo wa kwanza katika EPL.
Man-City walisajili ushindi wa 1-0 katika mechi hiyo iliyochezewa uwanjani Wembley.
Ratiba ya Uefa (Jumanne, Aprili 9, 2019):
Spurs na Man-City
Liverpool na FC Porto
(Jumatano, Aprili 10, 2019):