Makala

Faida za mapapai kiafya, kimapato na upanzi

April 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

WATAALAMU wa afya wanashauri usikose angalau tunda ama mawili mezani wakati wa mlo.

Matunda yamesheheni madini mbalimbali, na yanafahamika kwa kiini kizuri cha Vitamini.

Kuna matunda ainati kama vile; machungwa, ndizi, matufaha, maembe, maparachichi, mapapai, karakara na mapera, haya yakiwa machache tu kuorodhesha.

Katika makala hii, tunaangazia tija za mapapai na namna ya kuyapanda.

Tunda la papai lina Vitamini A, B, C, D na E, hivyo basi tunda hili linaorodheshwa katika kundi la matunda na vyakula vyenye utajiri mkubwa wa Vitamini.

Kulingana na Mary Ann Njeri, mtaalamu wa afya, ni kwamba mbegu za mapapai hukabiliana na shida ya tumbo.

“Hutibu udhaifu wa tumbo kama vile kutosagika kwa chakula,” anasema Bi Njeri.

Wazazi hushauriwa kuwapa watoto wao mapapai kwa wingi, hasa wakiwa wadogo kwa kuwa matunda haya huwawezesha kuenda haja bila matatizo.

Aidha, matunda haya hayana asidi yakilinganishwa na machungwa, hivyo basi walio na shida ya asidi hupendekezwa kuyala kwa wingi.

Nchini Kenya, maeneo yanayojulikana kuyakuza kwa wingi ni Nyeri, Embu, Meru na Kirinyaga. Yanastawi katika udongo tifutifu na udongo wa kufinyanga.

Daniel Mwenda, mtaalamu wa masuala ya kilimo hasa matunda anasema yanahitaji udongo wenye uchachu wa wastani, pH 6.0-7.0.

“Ninahimiza mkulima kujua asidi na alkalini ya udongo wa shamba lake kabla ya kuanza kukuza mimea,” anashauri Bw Mwenda.

Kulinga naye ni kuwa ukuzaji wa mapapai hauna gharama ya juu. Mdau huyu anasema miche ya mapapai huchukua muda wa miezi miwili na nusu katika kitalu.

Upanzi

Mbegu za jinsia ya kiume na kike ni suala la kuzingatia, ambapo asilimia 95-98 inafaa kuwa kike na iliyosalia iwe ya kiume. Bw Mwenda anasema mbegu za mapapai huuzwa kulingana na  jinsia.

Miche ikikaribia kuwa tayari kwa uhamisho, mkulima anashauriwa aanze maandalizi ya shamba. Kipimo cha shimo moja hadi lingine kiwe na nafasi ya mita 2.5, na kutoka laini moja ya shimo hadi nyingine iwe na kipimo sawa na hicho.

Urefu wa shimo kuenda chini unategemea aina ya udongo na kimo cha mche. Mwenda anasema udongo tifutifu unahitaji shimo lenye urefu wa futi 1 kuenda chini, na upana wa futi 1.5.

Anaendelea kueleza kwamba mashimo ya udongo wa kufinyanga yawe na urefu wa nusu futi kuenda chini na upana wa kipimo sawa na hicho.

Mipapai inanogeshwa na mbolea hai. Udongo wa juu uchanganywe na mbolea, mchanganyiko huo urejeshwe shimoni hadi karibu nusu futi. Catherine Nyokabi, mtaalamu wa kilimo na mkulima wa mapapai Nyeri na Laikipia, anasema miche ipandwe kisha imwagiliwe maji. “Nafasi iliyosalia ni ya nyasi za boji (mulching), kwa minajili ya kuzuia uvukuzi wa maji hasa wakati wa jua kali,” anasema Bi Nyokabi.

Miche inayopaswa kupandwa ni yenye urefu wa karibu futi moja.

Baada ya upanzi, mipapai itunzwe kwa maji na mbolea ya mifugo ili kuinawirisha. Isitoshe, nafasi iliyoko kati ya mti wa matunda inaweza kupandwa mimea yenye madini ya Nitrojini, kama vile maharagwe.

Bw Mwenda anasema ni nadra mapapai kuathiriwa na magonjwa. Hata hivyo, magonjwa kama Pawpaw ring Virus na Bacterial wilt hushuhudiwa iwapo mkulima hakabiliani na makwekwe shambani.

Mdudu aina ya Tiripsi ndio hushambulia mapaipai. Kukabiliana na changamoto za magonjwa na wadudu, mkulima anahimizwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa kilimo au katika maduka ya kuuza bidhaa za kilimo.

Mazao

Ekari moja inasitiri kati ya mipapai 800-900. Kwa msimu, mpapai huzalisha zaidi ya kilo 40. Kilo moja sokoni inagharimu Zaidi ya Sh40, ingawa inategemea msimu na maeneo. Ni muhimu kutaja kwamba mipapai huanza kuzalisha matunda kuanzia mwaka wa pili baada ya upanzi.

Mbali na kuliwa, mapapai hutumika kuzalisha sharubati kwa kuchanganya na matunda mengine kwa njia ya kupondaponda kutumia blenda.

Kuna kampuni zinazounda juisi yake kwa kutumia mashine maalumu za kuunda sharubati.