Michezo

Kocha matumaini Shujaa watang'aa Singapore Sevens

April 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Paul Murunga wa kikosi cha Shujaa, ni mwingi wa matumaini kwamba kikosi chake kitajinyanyua zaidi katika duru ijayo ya Raga ya Dunia itakayoandaliwa jijini Singapore, Malaysia mwishoni mwa wiki hii.

Timu hiyo ya Kenya ya Raga ya wachezaji saba kila upande imepangwa katika Kundi C kwa pamoja na ‘C’ Uingereza, Wales na Amerika ambayo kwa sasa inanolewa na aliyekuwa mkufunzi wa Shujaa, Mike Friday.

Shujaa wameshuhudia panda-shuka tele katika kampeni zao za msimu huu, huku matokeo yao duni yakiwaweka katika hatari ya kuteremshwa daraja kwa wakati fulani kabla ya kivumbi cha Hong Kong 7s nchini China wikendi iliyopita.

Eroni Sau (kushoto) wa Fiji akabiliana na Nelson Oyoo wa Kenya kwenye Hong Kong Sevens Aprili 8, 2018. Picha/ AFP

Hata hivyo, itawalazimu vijana wa Murunga kujizatiti vilivyo na kusajili matokeo bora nchini Malaysia ili kukwepa kuangushiwa shoka ambalo pia linawakodolea.

Shujaa waliotawazwa mabingwa wa raga ya Singapore Sevens mnamo 2016 kwa sasa wanashikilia nafasi ya 13 kwa alama 23.

Ni pointi mbili pekee ndizo zinazowatenganisha na Japan waliopo nyuma yao.

Wales wanaojivunia alama 20 pekee, wanakokota nanga mkiani mwa jedwali la ligi hii ya mataifa 15.

Kwa mujibu wa kanuni za mapambano haya ya raga ya dunia, timu itakayokamata ligi hii ya duru 10 itadondoshwa kwenye orodha ya mataifa yanayoshiriki duru zote na kuhitajika kushiriki upya mchujo wa dunia mnamo 2020 ili kuweka hai matumaini ya kurejea kiputeni.

Amerika inaongoza jedwali la raga ya dunia kwa alama 130 baada ya kutinga fainali kwenye duru zilizoandaliwa Dubai, Cape Town, Hamilton na Sydney; kisha kutamalaki duru ya Las Vegas kabla ya kuambulia nafasi ya nne jijini Vancouver, Canada.

Mwishoni mwa wiki jana, kikosi hicho cha Friday kinachotarajiwa kuwa na kibarua chepesi katika Kundi C jijini Singapore, kiliambulia nafasi ya tatu jijini Hong Kong.

Uingereza ambayo imejizolea alama 90, inatazamiwa kutegemea zaidi makali na huduma za Dan Norton anayejivunia rekodi ya mfungaji bora na mwanaraga mwenye miguso mingi.

Kukamilika kwa duru ya Singapore, kutapisha duru mbili za mwisho wa msimu huu zitakazoandaliwa jijini London na Paris Mei 2019.

Wakiwa Hong Kong, Shujaa walichabangwa 22-5 na Fiji kabla ya New Zealand na Australia kuwapokeza vichapo vya 36-0 na 28-12 mtawalia.

Matokeo hayo yaliwateremsha katika shindano la kuorodhesha timu katika nafasi za tisa hadi 16.

Katika jumla ya duru saba zilizopita za Raga ya Dunia, Shujaa wameshindwa kupiga hatua na kufikia robo-fainali za kuwania Kombe Kuu la Raga (Main Cup).

Mbali na kuvuta mkia katika duru ya Vancouver Sevens, walipoteza mechi tano mfululizo kwa kupepetwa 47-7 na Australia katika robo-fainali ya Challenge Trophy na 22-14 dhidi ya Japan katika nusu-fainali ya kutafuta mshindi wa nambari 13 hadi 16.

Awali, walizabwa na Fiji (36-12), Samoa (35-12) na Canada (36-21) mechi za makundi.

KUNDI A: Fiji, Afrika Kusini, Scotland, Canada
KUNDI B: Ufaransa, Argentina, Australia
KUNDI C: Amerika, Uingereza, Kenya, Wales
KUNDI D: Samoa, New Zealand, Japan, Uhispania