• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Lugha ya kimataifa ikiwemo sifa zinazoibainisha

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Lugha ya kimataifa ikiwemo sifa zinazoibainisha

Na MARY WANGARI

HII ni lugha ambayo imevuka mipaka ya taifa na hivyo basi inatumiwa katika mawasiliano kimataifa.

Lugha ya kimataifa ni lugha ambayo inatekeleza majukumu ya kimataifa katika mawanda ya kisiasa, biashara ya kimataifa, ubadilishanaji wa utamaduni katika kiwango chakimataifa na katika sayansi na teknolojia, kwa mfano, Kifaransa, Kiitaliano, Kingereza, Kireno na lugha nyinginezo.

Sifa za Lugha ya Kimataifa

Hutumika katika vyombo vingi vya habari katika pembe nyingi kote ulimwenguni.

Sharti iwe inaweza kutimiza majukumu ya kimataifa.

Majukumu haya ni kama vile kidiplomasia, biashara, elimu, na usafiri.

Majukumu haya ni sharti yawe yanahusisha mataifa mbalimbali na yenye lugha tofauti tofauti.

Sharti iwe ni lugha inayosemwa na watu wengi katika pembe nyingi za dunia.

Lazima lugha hiyo iweze kujitokeza kama lugha unganishi katika mambo yanayohusu ubadilishanaji wa kiutamaduni baina ya jamii.

Nao utamaduni unahusu mambo mengi kama vile vifaa vya ujenzi, vya upishi, vya muziki na kadhalika.

Utamaduni pia waweza kuwa wa kimazingira, kijamii, kidini, kisiasa, au kiutawala.

Sauti ya Amerika (VoA), Radio Deutshe Welle (Ujerumani), Radio Transvaal (Afrika Kusini), na AllIndia Radio ni baadhi tu ya vituo vinavyosifika kwa matangazo kwa kurusha matangazo kwa lugha ya Kiswahili.

Lugha hii ya kimataifa hufundishwa katika vyuo vikuu vingi duniani.

Vyuo hivi ni kama vile vya Afrika Mashariki na Kati ambavyo vinafundisha Kiswahili kama somo la shahada.

Kiswahili kinafundishwa pia katika vyuo vikuu vingine vya Afrika Magharibi, Amerika, Ujerumani, Uswidi, Uingereza, Ujapani, Uingereza na kadhalika.

Hutumika kutangazia na idhaa nyingi kote duniani kuanzia Afrika ya Mashariki, Afrika ya Kati, Uingereza, Ujerumani, Ujapani, Uchina, na India. Idhaa hizi ni kama vile Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Kuunganisha

Ili lugha kuwa ya kimataifa, ni sharti iweze kuwaunganisha watu wanaoongea lugha ‘hafifu’.

Hapa ina maana ya kuwa lugha ambazo hazikua sana kiutamaduni kama nyingine na hizi lugha hafifu ni lugha ambazo hasa ni za watu wa mataifa ambayo hayajaendelea sana kiutamaduni.

Ni lugha inayotumika kuendeshea mikutano na shughuli rasmi zakimataifa.

Kiswahili ni moja kati ya lugha zinazotumiwa kama lugha rasmi katika mikutano ya Umoja wa Afrika.

[email protected]

Marejeo

Massamba, D.P.B. (2002). Historia ya Kiswahili 50 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Ipara, I. O. & Waititu, F.G. (2006). Ijaribu na Uikarabati. Nairobi: Oxford University Press.

Habwe, J. (2006). Darubini ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.

Maddo, U. & Thiong’o, D. (2006). Mazoezi na Udurusu: Kiswahili 102/2. Nairobi: Global Publishers.

You can share this post!

KIZAAZAA: Fataki Emirates Arsenal wakitoana kijasho na...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Simo/ Misimu katika jamii...

adminleo