Habari

Wakazi wa Ruiru wahimizwa kuzingatia lishe bora ili kuimarisha afya

April 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Ruiru wamehimizwa kupunguza siasa na kujihusisha na ujenzi wa taifa.

Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara alisema Alhamisi kwamba ili kufanikisha ajenda nne muhimu za serikali, ni sharti kupunguza siasa na kuchapa kazi mara moja.

“Wakati wa siasa sio sasa na kwa hivyo ni vyema kujihusisha na maswala yanayomsaidia mwananchi wa kawaida,” alisema Bw King’ara.

Aliyasema hayo wakati wa kuzindua mpango wa matibabu ya bure yaliyoendeshwa katika shule ya msingi ya Matopeni mjini Ruiru.

Zaidi ya wagonjwa 1,000 walipokea matibabu katika hafla hiyo iliyoendelea mchana kutwa.

Wauguzi wapatao 112 walijumuika pamoja kuwakagua wagonjwa waliofika kwenye kituo hicho.

Alisema uchunguzi uliofanywa ulibainisha ya kwamba watu wengi wanapata maradhi tofauti kwa sababu ya kukosa  lishe bora mwilini.

“Ni vyema watu kubadilisha msimamo wao wa kula chakula chao. Sio vyema kula chakula sampuli moja kila siku. Ni vyema kubadilisha na kula kile chenye afya bora,” alisema Bw King’ara.

Baadhi ya Mashirika na kampuni zilizofadhili mpango huo ni Tai Sacco, Equity Bank, KCB, Jet Lack, Familiy Bank, Ruiru Hospital na Neno Optician.

Kiongozi huyo aliwahimiza wakazi wa Ruiru kujiandikisha kwa Huduma Namba ili baadaye waweze kupata huduma kwa njia rahisi.

“Maneno yanayosemwa na watu kuwa kujiandikisha inaashiria mambo mengine ya kishetani sio kweli kwani wale wanaoleta uvumi huo ni wale wanapotosha wananchi,” alisema Bw King’ara.

Dkt Mercy Marangu ambaye ni mtaalamu wa lishe bora aliwashauri wakazi wa Ruiru kuzingatia kula vyakula vya afya ili kujiepusha na maradhi mengi.

 

Muuguzi amhudumia mgonjwa aliyefika kwa matibabu ya bure katika shule ya msingi ya Matopeni mjini Ruiru. Picha/ Lawrence Ongaro

“Kile kinachosababisha wengi wetu kupata maradhi tofauti mwilini ni kutokula vyakula vifaavyo mwilini. Kwa hivyo, ninawahimiza muwe makini na kula ipasavyo,” alisema Dkt Marangu.

Alitaja ugali, wali na viazi kama muhimu kwa kuongeza nguvu mwilini. Pia aliwashauri kula samaki, nyama, mayai, maharage na hata pojo ili kuongeza protini mwilini.

Wagonjwa wengi waliotibiwa walipatikana wakiugua kisukari, damu kuchemka, homa ya matumbo, kuharisha, na hata wengine walipatikana na saratani ya sehemu za siri kwa wanaume.

Ilidaiwa wanawake wengi hawafuatilii vyema lishe bora ya watoto wao kwa sababu wengi huwapa uji na chai bila kujua hiyo haina umuhimu kwa mwili wa mtoto.