Tanzania yapokeza Kenya-U17 kichapo cha magoli 3-2 soka ya UNAF U18
Na GEOFFREY ANENE
MABAO kutoka kwa Isaiah Abwal na Kevington Machika hayakutosha kuepushia Kenya kichapo cha tatu mfululizo kwenye soka ya Muungano wa Vyama vya Soka vya Kaskazini mwa Afrika (UNAF) ilipopigwa 3-2 na Tanzania uwanjani Tolip mjini Alexandria nchini Misri, Ijumaa.
Kenya, ambayo iliingia gozi hili la Afrika Mashriki ikiwa juu ya Tanzania kwa kutofungwa mabao mengi licha ya wote kuwa bila alama, saa inashikilia mkia bado ikitafuta alama yake ya kwanza.
Vijana wa kocha Michael Amenga watakamilisha ziara ya Misri dhidi ya Morocco mnamo Jumapili saa kumi na robo jioni.
Watahitaji ushindi wa zaidi ya mabao mawili ili kumaliza juu ya Tanzania, ambayo tayari imekamilisha mechi zake.
Kenya na Tanzania, ambazo zimealikwa, zilikosa majibu katika mechi zao zilizotangulia kwenye soka hii ya mataifa matano.
Vijana wa Amenga walilimwa 1-0 na Misri, huku Algeria ikipepeta Tanzania 3-1 katika siku ya kwanza mnamo Aprili 6 uwanjani Tolip unaobeba mashabiki 5,000.
Majirani hawa pia walipoteza Aprili 10 pale Algeria ilipokung’uta Kenya 5-1 nayo Tanzania ikalizwa 4-1 dhidi ya Morocco. Tanzania pia ilipoteza 2-0 dhidi ya Misri mnamo Aprili 8.
Mkenya Alphonse Omija alilishwa kadi nyekundu dhidi ya Algeria katika mechi ambayo Kenya ilipata bao lake la kwanza baada ya Mathew Mwendwa kuchana nyavu mara moja.
Kichapo dhidi ya Tanzania ni cha pili mfululizo kwa Kenya dhidi ya majirani wake waliowashinda 2-1 Aprili 25 mwaka 2018 katika nusu-fainali ya soka ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA U/17) nchini Burundi.
Misri na Morocco zinatarajiwa kulimana katika soka ya UNAF baadaye Ijumaa.
Timu itakayomaliza soka hii ya mataifa matano yanayotumia mfumo wa mzunguko itatawazwa bingwa.