Michezo

Kenya yaumizwa 2-0 na Morocco soka ya UNAF Misri

April 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imekamilisha soka ya Muungano wa Vyama vya Soka vya Kaskazini mwa Afrika (UNAF) kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 18 bila ushindi baada ya kupoteza mechi yake ya nne mfululizo kwa kuchapwa 2-0 na Morocco mjini Alexandria nchini Misri,  Jumapili.

Vijana wa kocha Michael Amenga walianza kampeni yao kwa kupigwa 1-0 na wenyeji Misri mnamo Aprili 6. Walipoteza mechi ya pili 5-1 dhidi ya Algeria mnamo Aprili 10 katika mechi ambayo Mathew Mwendwa alifungia Kenya bao la kufuta machozi.

Kenya ilipigana vikali dhidi ya majirani Tanzania kabla ya kusaliamu amri kwa mabao 3-2 Aprili 12. Apoel Izaye na Kevington Machika walifungia Kenya naye Mostafa Kandoro Hames akapachika mabao yote ya Tanzania.

Kwingineko, timu ya Kenya ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 16 iliratibiwa kuondoka nchini Jumapili kueelekea nchini Uhispania kwa soka ya Mediterranean International Cup (MIC Cup).

Timu ya Kenya ya soka ya Muungano wa Vyama vya Soka vya Kaskazini mwa Afrika (UNAF) kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 18. Picha/ Hisani

Timu hiyo inayonolewa na David Ouma itamenyana na timu za NT Terres na Junior CF kutoka Uhispania na Eastern FC kutoka Marekani katika Kundi D. Jumla ya timu 16 zitashiriki MIC Cup.