Chiellini kamanda wa Juventus aliye na hela kama changarawe
Na CHRIS ADUNGO
GIORGIO Chiellini, 34, ni nahodha na beki matata anayesakata gozi la kulipwa kikosini mwa wafalme wa soka ya Italia, Juventus. Ni miongoni mwa masogora wenye miguso ya kutamanika katika safu ya ulinzi ya timu ya taifa ya Italia.
Baada ya kuvalia jezi ya Livorno na AS Roma kati ya 1990 na 2003, umaarufu ulianza kumwandama Chiellini alipojipa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Fiorentina waliomsajili kwa kima cha Sh728 milioni mnamo 2004.
Ushawishi wake katika klabu hiyo ambayo ilijivunia huduma zake tangu akiwa kitoto cha miaka 16, ni miongoni mwa sababu ambazo ziliwachochea Juventus kumtia rasmi katika sajili yao mnamo 2005.
Akiwa baadhi ya walinzi wanaotegemewa pakubwa kambini mwa Juventus, Chiellini amewasaidia waajiri wake hao kutwaa ubingwa wa Serie A mara saba kati ya 2012 na 2016.
Ukomavu alionao pamoja na utajiri mkubwa wa kipaji chake ulimshawishi kocha Massimiliano Allegri kumwaminia Chiellini wadhifa wa nahodha wa timu ya Juventus baada ya kipa mkongwe Gianluigi Buffon kuyoyomea kambini mwa PSG nchini Ufaransa.
UTAJIRI
Thamani ya mali ya Chiellini inakadiriwa kufikia Sh6 bilioni na kiini kikubwa cha utajiri wake ni mshahara wa Sh28 milioni ambao kwa sasa anapokezwa na Juventus mwishoni mwa kila wiki. Awali, Fiorentina walikuwa wakimdumisha kwa mshahara wa hadi Sh20 milioni kwa wiki hadi kufikia mwishoni mwa msimu wa 2004-05.
Mbali na mshahara huo, Chiellini hujirinia fedha za ziada kutokana na matangazo ya kibiashara kila anapoteuliwa na kampuni mbalimbali awe balozi wa mauzo wa bidhaa ha huduma zao.
Aidha, sogora huyo hujipa hela nyinginezo kutokana na marupurupu ya kuzishinda mechi katika ngazi za klabu na timu ya taifa.
Kwa pamoja na Lionel Messi wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, Chiellini aliteuliwa mnamo 2013 kuwa balozi wa kuvumisha umaarufu wa bidhaa za kampuni za Electronic Arts (EA Sports) ambayo humkabidhi kila mmoja wao takriban Sh14 milioni kwa wiki. Kwa sasa, Chiellini ni balozi wa kutangaza bidhaa za kampuni ya Adidas ambayo humkabidhi takriban Sh35 milioni kila mwezi.
Hii ina maana kwamba hutia mfukoni zaidi ya Sh180 milioni mwishoni mwa kila mwezi. Kiasi hiki cha pesa kinamweka Chiellini katika kundi moja na Leonardo Bonucci, Blaise Matuidi, Emre Can, Miralem Pjanic, Sami Khedira, Paulo Dybala na Mario Mandzukic ambao ni miongoni mwa wanasoka mahiri wanaodumishwa vyema kifedha na na klabu ya Juventus.
Mwanzoni mwa msimu jana, Chiellini alitia saini kandarasi mpya ya miaka mitatu katika maelewano yatakayompa ulazima wa kuendelea kutoa huduma zake chini ya mkufunzi Allegri hadi mwishoni mwa msimu wa 2020.
MAGARI
Ingawa anamiliki magari mengi, Chiellini huvutiwa zaidi Ferrari F12 TDF, Audi Q9 na Lamborghini Gran-Turismo, magari ambayo kwa pamoja yamekadiriwa kumgharimu Sh70 milioni. Mkewe huendesha Jeep aina ya Wrangler S-SUV na Range Rover, magari ambayo yanakisiwa kuwa yenye thamani ya Sh22 milioni.
MAJENGO
Chiellini ana kasri la Sh375 milioni jijini Turin, Italia. Anamiliki pia jengo jingine la kifahari linalokisiwa kumgahrimu Sh320 milioni viungani mwa jiji la Palermo na moja zaidi alilolinunua jijini Pisa kwa kima cha Sh275 milioni mwishoni mwa 2012.
FAMILIA NA MAPENZI
Chiellini alizaliwa mnamo Agosti 14, 1984 jijini Pisa, Italia akiwa mmoja wa pacha katika familia ya Chieri na Andezeno ambao ni wafanyabiashara wa vipuri vya magari. Mapenzi ya Chiellini kwa soka yalijidhihiri akiwa na umri wa miaka minane pekee baada ya kujipa kazi ya kuwa ‘ball boy’ katika uwanja wa Stadio delle Alpi uliotumiwa na kikosi cha Sisport kufanyia mazoezi kabla ya kuhamia Livorno.
Ilikuwa hadi Julai 2014 ambapo Chiellini alifunga pingu za maisha na kichuna Carolina Bonistalli katika harusi ya kufana iliyoandaliwa katika kanisa Katoliki la Montenero jijini Livorno. Kwa pamoja, wawili hao wamejaliwa mtoto mmoja wa kike, Nina ambaye alizaliwa mnamo Julai 2015.