25/06/2019

Maguire, Lindelof na Reus madume ugani na chumbani vilevile

NA MWANDISHI WETU

BEKI matata wa Leicester City na timu ya taifa ya Uingereza, Harry Maguire, 26, sasa amekuwa dume kamili baada ya mkewe Fern Hawkins kujifungua mtoto wa kike kwa jina Lillie Saint.

Lillie alizaliwa wiki jana, miezi tisa tangu Uingereza iwachabange Colombia kupitia penalti kwenye hatua ya 16-bora ya fainali za Kombe la Dunia zilizoandaliwa nchini Urusi mnamo 2018.

Baada ya ufanisi huo, Maguire alifunga bao lililochochea Uingereza kuwabandua Uswidi kwenye robo-fainali ila wakazidiwa maarifa na Croatia katika hatua ya nne-bora.

Maguire anayehusishwa pakubwa na Manchester United, alimvisha Fern pete ya uchumba mnamo Februari 17, 2018 baada ya kutoka naye kimapenzi kwa zaidi ya miaka saba.

Mwanasoka mwingine aliyeingia rasmi katika kikoa cha wazazi wiki jana ni nahodha wa Borussia Dortmund, Marco Reus, 29.

Kwa pamoja na mchumba wake Scarlett Gartmann, 25, kiungo huyo wa timu ya taifa ya Ujerumani alijaliwa kimalaika cha kike.

Reus amekuwa akilidokoa tunda la Scarlett tangu 2015. Mkewe alifichua kuhusu hali yake ya ujauzito mnamo Oktoba mwaka jana baada ya kuanza kuhudhuria kliniki.

Kichuna huyo ambaye ni mpenzi mkubwa wa mbio za farasi, anajivunia zaidi ya mashabiki 300,000 kwenye mtandao wake wa Instagram.

Awali, beki wa Manchester United na timu ya taifa ya Uswidi, Victor Lindelof, 24 na mkewe Maja Nilsson pia walikuwa wamejaliwa mtoto wa kiume.

Maja alianza kumfungulia Lindelof buyu lake la asali mwishoni mwa 2012. Baada ya kumvisha kichuna huyu pete ya uchumba mwanzoni mwa Juni 2018, wawili hao walirasimisha uhusiano wao wa kipamenzi kupitia harusi ya kukata na shoka iliyoandaliwa jijini Stockholm, Uswidi mnamo Mei 2018.

Sherehe hizo za kufana ziliandaliwa mwezi mmoja kabla ya wachezaji wengine wa Man-United, Phil Jones na Chris Smalling kufunga pingu za maisha na warembo Kaya Hall na Sam Cooke mtawalia.