Michezo

IDCC kuamua kuhusu mechi ya Ingwe na SoNy Sugar iliyotibuka

April 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN ASHIHUNDU

Jopo Huru la Nidhamu na Malalamishi la KPL (IDCC) linatarajiwa Jumanne kutoa uamuzi kuhusu mechi iliyotibuka kati ya Sony Sugar na AFC Leopards.

Mchuano huo umeahirishwa mara mbili chini ya siku tatu zilizopita kwa sababu mbali mbali.

Jumapili, mechi hiyo ilisimamishwa dakika ya 68 kufutia mvua kubwa iliyonyesha mjini wakati Leopards walikuwa wakiongoza 1-0 lililofungwa na Whyvonee Isuza katika dakika ya sita.

Kulingana na sharia, mchezo huo ulikuwa urudiwe upya jana asubuhi kwa matokeo ya 0-0 katika uwanja huo huo wa Awendo Green Stadium.

Lakini haikucheza, baada ya Leopards kuwasili na kukataa kucheza huku wakilaumu wenyeji kwa kupuuza sharia za mechi za Ligi Kuu (KPL).

Akizungmza kuhusu pambano hilo, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Oscar Igaida alisema timu yake haikuhakikishiwa usalama wa kutosha kuambatana na sharia za Shirikisho la Soka Nchini (FKF).

“Kulkikuwa tu na maafisa wa usalama wane uwanjani wakati mechi hiyo ilitarajiwa kuanza. Mechi yoyote inayohusu AFC Leopards haiwezi kuchezwa bila maafisa wa polisi 20 kuwepo,” alisema Igaida.

“Kadhalika, ambulensi iliyokuwepo haikuwa na vifaa hitajika vya matibabu wala daktari. Wachezaji wetu wamekuwa wakijeruhiwa vibaya msimu huu kutokana na hali mbali ya viwanja mbali mbali, na kamwe hatuwezi kuendelea kuvumilia hali kama hii. Tunatarajia maafisa wa ligi watupe ushindi wa mechi hii.”

Hata hivyo, wakuu wa klabu ya Sony wamekanusha madai ya Igaida, huku wakiishutumu Leopards kwa kujitokeza na vijisababu kadhaa ili wasicheze.

“Walifika uwanjani leo huku wakijawa na sababu mbali mbali ziziso na msingi. Ni kweli walipata ambulensi ikiosa kifaa Fulani na wakasisitiza. Walitaka idadi ya maafisa wa polisi iongezeke ili wacheze, lakini wakalalamika na kuondoka. Natarajia KPL watatupatia ushindi ama waamrishe mechi ichezwe upya.”

Lakini kulingana na Afisa Mkuu wa KPL, kuna uwezekano wa mechi hii kurudiwa.

“Tutazungmza na aliyesimami mechi hiyo pamoja na marifarii wahusika. Wao ndio macho yetu na tutafuata watakachotuambia. Mechi zote zinaamliwa uwanjani. Nionavyo hiui mechi itachezwa siku nyingine,’ alisema Oguda.

Leopards wanakamata nafasi ya 12 jedwalini baada ya kujibwaga uwanjani mara 22 huku Sony wakikamata nafasi ya saba.

Gor Mahia, Bandari na Sofapaka wanafuata mtawaliwa kutoka kileleni huku Mount Kenya United na Zoo Kericho zikiendelea kubakia katika nafasi mbili mkiani.