MAPOZI: Azma Mponda
Na PAULINE ONGAJI
JINA lake sio geni katika ukumbi wa Hip Hop sio tu nchini Tanzania alikozaliwa, bali Afrika Mashariki kwa ujumla.
Alikuwa msanii wa kwanza wa mdundo huu Afrika Mashariki kutazamwa mara milioni moja kwenye mtandao wa YouTube.
Alipojitosa katika muziki kwa mara ya kwanza, Azma Mponda alijiundia jina kutokana na muziki wake uliojaa ujumbe mzito wa uhalisi wa maisha, mojawapo ya sababu zilizomtenganisha na wasanii wengine wa mdundo huo nchini mwao.
Kwa wasiomfahamu, Azma anafahamika kwa vibao kama vile Kidedea, Garagasha, Shubiliga alioimba kwa ushirikiano na Gilad, miongoni mwa vingine.
Kilichompa mvuto mwanzoni ulikuwa ujumbe mzito katika nyimbo zake, suala lililomfanya kudhaniwa kuwa na msimamo mkali.
Lakini licha ya kujivunia mashabiki kutokana na mdundo huu, ilimlazimu kulegeza kamba na kupunguza makali ya ujumbe wake kama mbinu ya kufikia soko jipya.
“Wajua awali nilikuwa naimba hip hop yenye ujumbe mzito, muziki ambao haukukubalika kabisa redioni na hivyo ilinibidi kupunguza makali kidogo na kutunga nyimbo ambazo zinahusisha mada za kufurahisha masikio kama vile mapenzi,” alisema kwenye mahojiano baada ya kurejea.
Kwa hivyo, mwaka wa 2016 alirejea baada ya kimya cha miaka mitatu huku akiwa na mkakati mpya wa kupunguza makali hayo, ambapo alianza kwa kuangusha kibao Astara Vaste alichoimba kwa ushirikiano na Belle.
Kama mbinu ya kuthibitisha uwepo wake katika jukwaa la muziki Afrika Mashariki, wakati huo alirejea akiwa na kikundi cha maprodusa na mapromota mbali na kuwa na usimamizi mzuri.
Hii kulingana naye ilikuwa mbinu ya kunasa mashabiki kutoka sehemu hizi zote hasa ikizingatiwa kwamba maprodusa hao walielewa muktadha wa nchi yao na hivyo wangemshauri kutunga nyimbo zinazofurahisha mashabiki katika nchi hizi tofauti.
Na haikuwa muda kabla ya mkakati huu kuanza kuzaa matunda kwani wakati huo alianzisha ziara mbalimbali hapa nchini, kwao Tanzania, na Uganda.
Pia, huo ulikuwa mwanzo wake wa kushirikiana na wanamuziki wa haiba ya juu kutoka humu nchini, Tanzania na Uganda.
Humu nchini, Azma ameshirikiana na wasanii kama vile Khaligraph Jones na Gilad. Nchini Tanzania ameshirikiana na wasanii kama vile Joseph Mbilinyi na Izzo Bizness miongoni mwa wengine, huku nchini Uganda akifanya kazi na mwanadada AVM kwenye kibao Whine Up.
Lakini haikuwa rahisi kwa Azma alipofanya uamuzi huu kwani alipowasili humu nchini ili kufanyia shughuli zake hapa, wengi walidhania kwamba kama wasanii wengine kutoka Tanzania waliofifia baada ya kuja Kenya, pia kwake hatima ingekuwa hiyo hiyo.
Lakini Azma ameenda kinyume na matarajio ya wakosoaji wake na kuzidi kung’aa huu ukiwa mwaka wake wa tatu tangu achukue uamuzi wake.
“Tatizo ni kuwa wasanii wanaokumbana na masaibu hayo wanapohamisha shughuli zao hapa Kenya huwa na tatizo la kusikiza ushauri. Wengi wao hawasikizi mapromota na maprodusa wao hivyo inakuwa vigumu kwao kunasa mashabiki kama inavyohitajika,” alisema katika mahojiano.
Pia, siri yake ya ufanisi ilikuwa mazoea yake ya kushiriki kwa kila kitu kinachofanywa kuhusiana na muziki wake, vile vile uhusiano wake mzuri na watu wote wanaohusika na muziki wake.
Huu ni mwaka wa tatu tangu Azma Mponda afanye uamuzi huu na huenda muda unavyozidi kusonga, atakuwa funzo kwa wenzake na kuwathibitishia kwamba inawezekana kuendesha shughuli katika mataifa yote ya Afrika Mashariki, na katika harakati hizo kunasa mashabiki.