18/07/2019

Thika Queens kuvaana na Gaspo KWPL

Na JOHN KIMWERE

MALKIA wa zamani katika Soka la Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL), Thika Queens wikendi hii watakuwa mbioni kuwinda alama sita muhimu ili kujiongezea tumani la kufanya kweli msimu huu.

Thika Queens Jumamosi itakuwa ugenini kucheza na GASPO Women kwenye mechi inayotazamiwa kushuhudia msisimko mkali itakayochezewa uwanjani Ruiru mjini humo.

Kisha Jumapili itarejea nyumbani kuialika Vihiga Leeds. Vihiga Leeds itacheza mchezo huo siku moja baada ya kukabili Makolanders uwanjani Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.

Thika Queens ya kocha Benta Achieng imejikuta njia panda msimu huu baada ya kudondosha mechi mbili.

“Tuna kibarua kigumu msimu huu wapinzani wetu wamejipanga kutubomoa lazima wachezaji wajitume kufa na kupona maana kwa wenzetu hakuna kulaza damu,” ofisa mkuu wa Thika Queens, Fredrick Chege alisema.

Thika Queens itashuka dimbani ikijivunia kushinda Soccer Queens kwa mabao 5-1 wiki iliyopita. Kikosi hicho kinategemea huduma za wachezaji mahiri akiwamo Catherine Wangechi, Rachael Mwema, Fauzia Omar na Mwanahalima Adams kati ya wengine. Nao mabingwa watetezi, Vihiga Queens itakwaruzana na Eldoret Falcons uwanjani Mumias Complex mjini humo.

Vihiga Queens ya kocha, Alex Alumira ingali kifua mbele kwenye msimamo wa kipute hicho kwa kuzoa lama 27, sita mbele ya Trasn-Nzoia Falcons na GASPO Women tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Kwenye ratiba ya michuano hiyo, Oserian Ladies itakaribisha Kisumu Allstars nayo Kayole Starlets itagarazana na Kibera Girls Soccer Academy (KGSA) uwanjani Barclays Sports Club Thika Road.

Habari zinazohusiana na hii

Leave a Reply