• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Serikali yatisha kuzimia wananchi simu

Serikali yatisha kuzimia wananchi simu

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imetishia kuzima laini za simu za Wakenya ambao hawatakuwa wamejisajili kwa mpango wa Huduma Namba baada ya kumalizika kwa muda uliotengewa usajili huo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CA) Francis Wangusi Alhamisi alisema ifikapo Mei 8, Wakenya ambao hawatakuwa wamejisajili kwa mfumo huo mpya wa kijiditali hawataweza kutumia huduma za simu za mkononi.

Hii ina maana kuwa, mtu hataweza kufikia huduma zifuatazo; kupiga na kupokea simu, kuwasiliana kwa mtandao wa WhatsApp, kutuma na kupokea pesa kwa njia M Pesa na Airtel Money na kutoa pesa kupitia mitambo ya ATM.

“Tutauliza kampuni za kutoa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi kuzima laini (SIM cards) za wale ambao hawatakuwa wamepata Huduma Namba muda wa usajili utakapoisha,” Bw Wangusi akasema.

Akaongeza: “Na wale ambao hawatakuwa na laini za simu hawataweza kununua laini mpya ikiwa hawana Huduma Namba.” Bw Wangusi alitoa tangazo hilo jana alipokuwa akiwahutubia wajumbe waliohudhuria maadhimisho ya wiki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) mjini Kisumu.

Lakini kwenye taarifa kwa vyombo vya habari jana, Mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu Nzoika Waita alifafanua kuwa Wakenya hawatashurutishwa kujisajili kwa Huduma Namba. Bw Waita alisema hakuna amri yoyote imetolewa na Serikali kuwaadhibu wale wasiojisajili. Badala yake, Wakenya wote watahamasishwa kuhusu umuhimu wa kuwa na Huduma Namba.

Shughuli ya usajili kwa Huduma Namba ilianza mnamo Aprili 2 na inatarajiwa kuendelea kwa siku 45, hadi tarehe 18 mwezi ujao. Shughuli hiyo ilizinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta katika kaunti ya Machakos wiki mbili zilizopita.

Mnamo Jumanne, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alitangaza kuwa kufikia sasa jumla ya Wakenya milioni tano wamejisajili kwa Huduma Namba huku akisema lengo la serikali kuhakikisha kuwa kila Mkenya aliyetimu miaka 18 amejisajili.

Jana, Bw Wangusi alisema zoezi hilo ni muhimu kwa sababu ni zao la maendeleo katika nyanja ya teknolojia inayolenga kuharakisha utoaji huduma kwa wananchi.

“Shughuli hii ni muhimu lakini inasikitisha kuwa baadhi ya Wakenya hawaichukulii kwa uzito,” akasema.

Mkurugenzi huyo wa CA aliongeza Huduma Namba itaisadia serikali kubuni mbinu na mikakati ya kupambana na uhali inayoendeshwa mitandaoni na hivyo kuzuia hasara zinazotokana na maovu hayo.

“Watu wengine wanaweza kushuku nia ya serikali kuanzisha mpango huu, lakini serikali imejitolea kuzima uhalifu mitandaoni huku ikilinda data za watu na siri zao,” akawaambia wajumbe hao huku akiongeza kuwa visa vya watu kujisali kwa M-Pesa kutumia majina feki pia vitazima kupitia Huduma Namba.

Bw Wangusi alisema kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumia mianya katika sheria na kujisajili kwa Mpesa na huduma nyinginezo za simu kwa kutumia majina bandia.

Tishio la Bw Wangusi linakwenda kinyume na agizo Mahakama Kuu kwamba, Wakenya wasilazimishwe kujisajili kwa zoezi hilo.

You can share this post!

JOHN OGO: Msanii ibuka anayelenga kuwapa matumaini...

Simanzi na majonzi Wangechi akizikwa

adminleo