Ruto: Wakenya si wajinga 'kiasi hicho'
Na CHARLES WASONGA
NAIBU Rais William Ruto ameonekana kumjibu Rais Uhuru Kenyatta kuhusu kauli ya kwamba ushirikiano wake na kiongozi wa ODM Raila Odinga hauna uhusiano wowote na siasa za mwaka 2022 bali masuala yenye umuhimu kwa Wakenya.
Akionekana kumrejelea Rais, Dkt Ruto alilalamika kuwa kuna watu “mahali fulani ambao wanawachukulia Wakenya kama wajinga”.
Watu ambao, alisema, aidha wanadhani Wakenya hawajui kinachoendelea au wanaamini kuwa Wakenya hawajui nani atakuwa Rais wao.
“Kuna watu fulani ambao wanadhani Wakenya ni wajinga. Wakenya wanajua ni nani atakuwa Rais wao. Koma kutuletea siasa. Kuna uhaba mkubwa wa wajinga nchini,” Ruto akasema Ijumaa alipohutubu katika hafla ya Kanisa mjini Nyeri.
Mnamo Jumatano jioni Rais Kenyatta aliwakashifu wanasiasa wandani wa Dkt Ruto ambao wamekuwa wakimshambulia Bw Odinga wakidai yeye (Raila) ndiye chimbuko la misukosuko ndani ya Jubilee.
Wabunge hao wanamtaka Rais Kenyatta kuvunja uhusiano wake na Bw Odinga.
Hata hivyo, Rais amekuwa akishikilia kuwa hakuna kitakachomtenganisha na kiongozi huyo wa ODM akitoa wito kwa wandani hao wa Ruto kutafuta kitu kingine cha kufanya.
Dkt Ruto amejitenga na muafaka kati ya Bw Odinga na bosi wake akisema unalenga kuvuruga azma yake ya kuingia Ikulu 2022.
“Nasikia baadhi ya watu wakizunguza katika mazishi na harusi wakisema ndugu yangu Raila anachochea migawanyiko ndani ya Jubilee kwa manufaa ya ndoto zake za urais 2022. Ningependa kufafanua kuwa hatujawahi kuzungumza kuhusu ODM au Jubilee. Hajawahi kuniambia kuwa atawania urais mwaka 2022 na mimi pia sijadokeza kuwa nitawania tena 2022.
“Mazungumzo hujikita katika masuala ya kufaidi Wakenya,” Rais akasema alipohutubu katika mkutano wa kujadili ufadhili wa ujenzi wa miundombinu barani Afrika.
Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.
“Binafsi hata sijui ODM ni nini,” Rais Kenyatta akaongeza.