UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Lahaja
Na MARY WANGARI
LAHAJA YA KIBARAWA
HII ni lahaja inayotumiwa na wazungumzaji wa Kiswahili katika eneo la katikati ya Mogadishu, Somalia. Lahaja hii huzungumzwa katika maeneoya Marka na Barawa, si ajabu baadhi ya wataalamu huizungumzia kama lahaja ya Kibarawa.
Kwa Mfano:
CHIMINI/ KIBARAWA | KISWAHILI SANIFU |
oloka | Ondoka, nenda |
Milu | Miguu |
Chintu | kitu |
Shikilo | sikio |
ikulu | kubwa, tukufu |
LAHAJA ZA KATI
KIMVITA
Hii ni lahaja inayozungumzwa katika kisiwa cha Mombasa au Mvita kama ilivyojulikana zamani. Lahaja hii ina sifa zinazokaribiana sana na za Kiamu.
Katika lahaja ya Kimvita, sauti ‘t’ inachukua nafasi ya sauti‘ch’ katika Kiswahili sanifu.
Kwa mfano:
KIMVITA | KISWAHILI SANIFU |
mtele | mchele |
mtuzi | mchuzi |
mwivi | mwizi |
vyaa | zaa |
mtanga | mchanga |
KIJOMVU/CHIJOMVU
Ni lahaja ambayo hutumiwa katika maeneo ya pembeni ya mji waMombasa, kaskazini nje ya kisiwa cha Mombasa.
Katika lahaja hii, maneno ambayo katika Kiswahili sanifu huanza kwa sauti ‘ki’ hubadilikana kuwa ‘chi’.
Kwa mfano:
KIJOMVU | KISWAHILI SANIFU |
Chiyana | kijana |
chichi | hiki |
chioo | kioo |
chamba | kwamba |
wenjine | wengine |
KINGARE
Ni lahaja inayosemwa Mombasa katika maeneo ya kiwanja cha ndege na Kilindini.
Kwa mfano:
KINGARE | KISWAHILI SANIFU |
nzee | mzee |
yakwe | yako |
geshi | jeshi |
LAHAJA ZA KUSINI
KIVUMBA
Hii ni lahaja ya Kiswahili ambayo huzungumzwa katika sehemu za Vangana Wasini (sehemu za kusini mwa Mombasa). Lahaja hii inaonyesha matumizi ya sauti ‘r’ badala ya ‘t’ katika Kiswahili sanifu.
Kwa mfano:
KIVUMBA | KISWAHILI SANIFU |
kuogova | kuogopa |
ngia | njia |
mroro | mtoto |
vira | pita |
rosini | sote |
CHICHIFUNDI/CHIFUNDI
Hii ni lahaja inayozungumzwa Shimoni au kaskazini mwa Vanga, kusini mwa pwani ya Kenya.
CHICHIFUNDI | KISWAHILI SANIFU |
vochea | pokea |
kadzi | kazi |
njisi | ngisi |
sichia | sikia |
KIMTANG’ATA
Hii ni lahaja inayozungumzwa katika eneo la pwani ya Mrima, Pangani na hata Tanga.
Ni lahaja inayoonyesha uhusiano wa karibu sana na lahaja ya Kimvita na Kijomvu.
Kwa mfano:
KIMTANG’ATA | KISWAHILI SANIFU |
oka | choma |
munyu | chumvi |
Fyoma | soma |
chama | hama |
Marejeo
Chiraghdin, S., & Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.
Richards, J.C., (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition. London: Longman Group Ltd.
Wardhaugh, R. (1986). An Introduction to Socio-Linguistics: New York: Blackwell Publishers.