Raha ya ndoa ni kutogawa asali, utafiti wathibitisha
NA BENSON MATHEKA
Siri ya kuwa na maisha ya furaha katika ndoa sio kuchagua mchumba mwenye mali, sura au umbo la kuvutia, ni kutokuwa na mipango ya kando, utafiti wa hivi punde umefichua.
Utafiti huo ambao ulifanywa kwa miaka mingi umefichua kwamba kuwa na wapenzi wengi kabla ya kuoa au kuolewa kunakosesha mtu raha katika ndoa.
Kulingana na utafiti huo, watu wanaofanya mapenzi na mtu mmoja katika maisha yao kabla na kwenye ndoa, hufurahia ndoa mara saba kuliko waliogawa na wanaozoea kugawa tunda.
“Hata kuwa na mpenzi mmoja au wawili kabla ya ndoa kunapunguza furaha katika ndoa,” unasema utafiti wa taasisi ya masuala ya kifamilia ya Amerika. Watafiti waligundua kuwa uaminifu katika ndoa una manufaa zaidi kwa mtu sio tu katika ndoa bali pia kuhusu masuala mengine ya kibinafsi maishani kisaikolojia, kimwili, kiafya na kiroho.
“Huo ndio ukweli wa mambo ambao watu wengi wanajua lakini wanapuuza,” asema Dkt Sally Saikou mshauri wa wanandoa katika kanisa la Liberty Live worship centre mjini Athiriver, Machakos.
Anakubaliana na utafiti kwamba jinsi watu wanavyofanya mapenzi kabla ya ndoa na watu tofauti, ndivyo wanavyopunguza furaha katika ndoa.
Kulingana na utafiti huo, mtu akivumilia na kufanya mapenzi baada ya ndoa huwa anajiheshimu na kuwa na furaha katika maisha yake ya baadaye.
Kwa mujibu wa utafiti mwingine wa chuo kikuu cha Utah, Amerika, sababu moja ni kuwa mtu ambaye amekuwa na mpenzi moja kabla ya ndoa, huwa vigumu kupata majaribu.
“Watu wanaojiachilia kwa mpenzi mmoja katika maisha yao hufurahia maisha ya ndoa mara saba zaidi kuliko wale walio na mipango ya kando,” asisitiza Profesa Wolfinger Notinghah, kiongozi wa utafiti huo.
Dkt Saikou asema japo watu wanaogawa asali nje ya ndoa hutoa sababu tofauti za kutetea tabia yao, huwa wanajikwaa katika maisha yao ya ndoa na kuhujumu raha yao binafsi.
Kulingana na utafiti wa chuo kikuu cha Utah, iliibuka kuwa asilimia 71 ya wanaume wasiochovya nje ya ndoa wanafurahia maisha ya ndoa. Asilimia 64 ya wanawake wasiogawa tunda nao walisema wanafurahia maisha ya ndoa na hawajuti kuwa waaminifu kwa wachumba wao.
“Kiwango cha ubora wa maisha ya ndoa hutegemea idadi ya wapenzi ambao mtu anashiriki tendo la ndoa nao kabla ya wakati wa ndoa. Wakiwa wengi, kiwango cha ubora hushuka na matokeo ni kutofurahia ndoa. Kudumisha uaminifu kunamaanisha furaha katika ndoa,” asema Saikou.
Profesa Notinghah asema kwamba kuwa na mpenzi mmoja maishani kunafanya mtu kuwa na maisha ya ndoa ya kuridhisha.
“Hii ni kwa sababu mtu huelekeza hisia, nguvu na moyo wake kwa mtu mmoja ambaye ni chaguo lake kuliko wanaofanya majaribu na watu tofauti kabla ya kuolewa,” asema.
Wataalamu wanasema kwamba watu wakiwa na tabia ya kugawa asali kabla ya ndoa huwa ni vigumu kuacha tabia hiyo wakiolewa jambo linalofanya ndoa nyingi kukosa furaha. Kulingana na Dkt Mary Kasumbi wa shirika Maisha Mema jijini Nairobi, tabia ya kuchepuka ya mwanandoa mmoja huwa inaathiri furaha ya mwenzake na ndoa yao.
“Kuwa na wapenzi nje ya ndoa, kuwa na wanawake wengi au wanaume kando na mume au mkeo kuna hatari nyingi zinazofanya ndoa kukosa ladha inayoleta furaha. Watu wanaposhauriwa kutofanya mapenzi kabla ya kuoana na nje ya ndoa ni kwa sababu ya athari za tendo hilo kiroho, kisaikolojia na kimwili. Raha ya ndoa ni kujihifadhi kwa mumeo au mkeo,” asema Bi Kasumbi.