GASPO wawashtua vipusa wa Thika KWPL
Na JOHN KIMWERE
MALKIA wa zamani, Thika Queens ilijikuta njia panda ilipozabwa mabao 4-3 na GASPO Women kwenye mechi ya Soka ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL) iliyochezewa uwanjani Ruiru Stadium mjini humo.
Thika Queens inayojivunia kushinda taji hilo mara tatu iliyeyusha mchezo wa tatu na kujiweka pabaya kwenye juhudi za kupigania taji hilo ililolikosa msimu miwili iliyopita.
Wachana wavu wa GASPO Women washuka dimbani kwa kasi wakilenga kufunza wapinzani wao jinsi ya kucheza kandanda na kujiongezea alama zote muhimu.
Elizabeth Wambui alitangulia kuiweka GASPO Women kifua mbele kabla ya Fauzia Omar kujifunga na kuiongezea bao la pili. Kisha Salome Akoth alifungia Thika Queens ya kocha Benta Achieng na kufanya GASPO Women maba 2-0 kufikia muda wa mapumziko.
Kipindi cha pili GASPO Women ilirejea dimbani kwa kishindo huku Wincate Kaari akifaulu kucheza na wavu mara mbili kabla ya Mwanahalima Adams na Nuru Hamadi kufungia Thika Queens bao moja kila mmoja.
”Itabidi wachezaji wangu wazinduka maana tayari tumepoteza mwelekeo bila shaka itakuwa vigumu kufukuzia mahasimu wetu ambao hadi sasa hawajapoteza mchezo wowote,” ofisa mkuu wa Thika Queens, Fredrick Chege alisema.
Nao wachezaji wa Makolanders walituzwa ushindi wa mezani wa alama zote bila jasho baada ya Vihiga Leeds kuingia mitini. Naye mchezaji wa Kisumu Allstars Bertha Omita alitikisa wavu mara moja kabla Oserian Ladies kusawazisha kupitia Leila Opiyo kwenye mechi iliyokamilika sare ya bao 1-1.