Joylove sare, mabinti wa Mukuru warudi Nairobi kwa raha
Na JOHN KIMWERE
TIMU ya wanawake ya Sunderland Samba ilijikuta njia panda mbele ya Joylove FC huku Mukuru Talent Queens ikicharaza Moving The Goalposts (MTG) United kwa mabao 3-2 kwenye mechi ya Soka kuwania Ligi ya Taifa Daraja ya Kwanza iliyopigwa mjini Mombasa.
Mukuru Talent Queens ya kocha Amos Abong’o ilirejea jijini Nairobi kwa tabasamu baada ya kuvuna alama tatu ugenini kwenye utangulizi wa kampeni zake msimu huu.
Mchezo huo haukuwa mteremko na vigoli hao walipata shughuli zito mbele ya wenyeji wao waliokuwa wakishabikiwa na wafuasi wa nyumbani.
Mukuru Talent ikiongozwa na nahodha, Belinda Awour ilitwaa ushindi huo kupitia jitihada zao Amina Musindi, Carolyne Simiyu na Shangila Ramadhan waliotinga bao moja kila mmoja.
”Tumeanza michezo yetu vizuri licha ya kuzoa ushindi mwepesi,” kocha wa Mukuru Talent Queens alisema.
Sunderland Samba ilitoka chini mabao 2-0 na kujituma kiume kabla ya kukubali kutoka sare ya magoli 3-3 dhidi ya Joylove ilionekena kuja kivingine msimu huu.
Wafungaji wa Sunderland Samba walikuwa Irene Aluoch, Sylvia Akoth na Elizabeth Majuma waliopiga moja safi kila mmoja.
Kwa Joylove FC Faith Evayo alitingia mabao mawili huku Pesah Naliaka akicheka na wavu mara moja. Nayo Limuru Starlets ililala kwa mabao 2-1 na Soccer Sisters.