Jonathan Toroitich: Mwana wa hadhi aliyekuwa na roho ya utu
Na MWANGI MUIRURI
IKIWA kuna mwana wa Rais Mstaafu, Daniel Arap Moi ambaye aligusa nyoyo za wengi maishani, basi ni Jonathan Toroitich ambaye aliaga dunia mwishoni mwa wiki jana baada ya kuugua saratani ya maini.
Mwanasiasa mkongwe Koigi wa Mwere anasema kuwa mwendazake alikuwa mtu wa maisha ya kawaida mtaani na ambaye hata ungemuona akitembea kwa miguu akijiingiza katika mijadala na raia wa maisha ya chini.
“Hapa Nakuru alikuwa na biashara yake ya Supreme Furnitures na ambapo ungempata akitembea kwa miguu akijadiliana na raia. Hungemtambua ikiwa humjui… Ni mfano bora na tosha wa jinsi ya kuwa na hadhi maishani na ukwasi wa utu maishani vilevile. Tutamkosa hapa Nakuru,” akasimulia Koigi.
Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri anamkumbuka mwendazake kama rafiki wa wengi, msaidizi na mkarimu na ambaye hangekosa kukupa sikio lake ukimwendea kwa ushauri au usaidizi.
“Huyu alikuwa mlezi wa wengi… Alipendwa na mauti yake yametugusa nyoyo. Si kitu kwa kuwa yote ni ya Mungu… Lakini tungeambiwa tupige
kura dhidi ya mauti yake, tungemnusuru kwa kuwa kwa asilimia 100 alikuwa mwema kwetu,” anasema Ngunjiri.
Katika kijiji cha marehemu cha Kabimoi katika viunga vya Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo ni hapo ndipo palikuwa ngome yake na ambapo ameaga
dunia akiwa na umri wa miaka 66 na kifungua mimba wa Rais mstaafu.
Akifahamika kama JT, ilikuwa wazi katika Kaunti hiyo kuwa kunaye aliyekuwa ameaga na kuwashtua wenyeji kwa msiba si haba, huku
viongozi wa kitaifa wakizidisha kutuma risala zao za rambirambi kwa familia ya mwendazake.
Kujulikana
Huyu JT alikuwa akitesa katika safu ya mbio za magari miaka ya 1980 na ambapo alijulikana sana na mashabiki wa mashindano hayo duniani.
“Hebu tafakari hayo… Mwana wa Rais akiwa katika mbio za magari na ambapo kwa kawaida hawezi akapewa ulinzi kama ule ambao tunashuhudia
wana wa marais wengine wakiandamana nao katika maisha yao ya kila siku… Inakudhihirishia kuwa Jonathan amekuwa kwa muda mrefu mtu wa
kupenda maisha ya kawaida licha ya kuwa na uwezo wa kujipa ushawishi mkuu kwa msingi wa mizizi ya familia yake,” asema.
Anahusishwa na miradi si haba ya maendeleo katika kaunti nyingi za Rift Valley na pia akiwa wa kuchangia washirika wake wa kimaisha waliokuwa wamealikwa kushiriki michango ya maendeleo kote nchini.
Ametajwa kama mweledi wa kibiashara na ambaye alishikilia uadilifu mkuu maishani mwake.
“Alikuwa na uwezo wa kutumia jina la familia yake kujipa mali hata kama ni kutumia mbinu na njia za mkato, akini alikaidi msukumo wa aina hiyo na ndipo akawa wa kubakia na yake ya haki na kugawana na wengine bila ubaguzi, na Mungu amrehemu katika maisha yake mapya,” asema.
Mwaka wa 2002 aliwania ubunge wa Eldama Ravine lakini akaambulia patupu, hali ambayo inazua kinaya cha kushabikiwa kama mpenda watu,
mkarimu na mwenye utu, lakini yakifika maamuzi ya kumpa huyo kazi ya uwakilishi kisiasa, wanamuangusha.
Ujasiriamali wake ulinoga katika safu za kilimo, ujenzi na sekta ya bima.
Seneta wa Baringo Gideon Moi ni ndugu yake mwendazake pamoja na Jennifer, John Mark, Raymond, Philip, June, na Doris Moi.
Huku kifo chake kikiwa kimeanza tayari kuchezewa siasa za ubabe eneo hilo la Rift Valley, ambapo kumekuwa na siasa za kuchuja nani afikie
familia hiyo na wale wa kuzimwa wasiifikie, ni matumaini ya wengi kuwa heshima zake za mwisho kutoka kwa wanaompenda hazitaathirika, na roho
yake ikiwa imetangulia mbele ya haki, itapata utulivu mwili ukizikwa.