Michezo

GOZI KALI: Fataki kulipuka ugani Old Trafford wenyeji Manchester United wakivaana na City

April 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MASHABIKI wa soka kote duniani wataelekeza macho yao ugani Trafford leo Jumatano usiku wakati wenyeji Manchester United watakapokabiliana na miamba Manchester City kwenye gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Man-United watakuwa mbele ya mashabiki wao, siku chache tu baada ya kupokea kichapo cha 4-0 dhidi ya Everton, na watakuwa wakipambana na timu inayokaribia kuhifadhi ubingwa ligi hiyo.

Ushindi kwa Man-United utawarejeshea matumaini ya kumaliza miongoni mwa nne bora, lakini pigo kwa wapinzani wao ambao wanafukuzana unyo unyo na Liverpool katika vita vya kuwania taji la msimu huu. Man-United walipata nafuu baada ya timu za Arsenal, Chelsea na Tottenham kupoteza pia pointi muhimu mwishoni mwa wiki jana.

Arsenal walizamishwa 3-2 na Crystal Palace uwanjani Emirates, Chelsea wakaagana na Burnley kwa sare ya 2-2 ugani Stamford Bridge huku Tottenham wakipepetwa 1-0 na Man-City uwanjani Etihad.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer atamkaribisha leo kikosini beki Luke Shaw ambaye amekuwa nje kutokana na adhabu ya Shirikisho la Soka la Uingereza (FA), lakini Phil Jones ataikosa mechi hiyo kutokana na jeraha alililopata wakicheza dhidi ya Everton.

Ander Herrera, Eric Bailly na Antonio Valencia watendelea kuuguza majeraha yao, lakini huenda Alexis Sanchez akaanza baada ya kupata nafuu kutokana na jeraha la goti.

Kwa upande wa Man-City, kocha Pep Guardiola atapanga kikosi chake bila ya kujumuisha nyota Kevin De Bruyne pamoja na kipa Claudio Bravo.

Vijana wa Guradiola wamo katika hali nzuri kwa sasa, lakini matumaini yao ya kutwaa mataji manne kwa mpigo msimu huu yalivurugwa na Tottenham waliowaondoa katika michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA) majuzi.

Tayari wametwaa ubingwa wa Carabao Cup na watakutana na Watford katika fainali ya Kombe la FA ugani Wembley mnamo Mei.

Ligini, hawajapoteza pointi yoyote tangu wapokee kichapo cha 2-1 dhidi ya Newcastle United mwezi Januari 2019, wakijivunia ushindi mara 10, ushindi wao wa mwisho wa 1-0 ukipatikana dhidi ya Spurs.

Kuhifadhi ubingwa

City wanaelewa vyema kwamba iwapo wataendelea kuandikisha ushindi, watahifadhi ubingwa wa EPL msimu huu.

Liverpool pia wako na nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo iwapo watendeleza matokeo mema katika mechi zilizobakia. Liverpool wanaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi mbili, lakini wamecheza mechi nyingi.

Man-United wanahitaji ushindi ili wafufue matumaini ya kufuzu kwa michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya msimu ujao. Man-United wanajivunia ushindi mara 72, sare 52 na kushindwa mara 52. Walishinda 3-2 uwanjani Etihad msimu uliopita, baada ya kutoka nyuma.

Lakini mchezo wao ugani Old Trafford umekuwa haivutii katika siku za karibuni, tangu waandikishe ushindi uliowapa taji la Leaue Cup mnamo Oktoba 2016.

Waliandikisha ushindi wa 4-2 mnamo Aprili 2015 kutokana na mabao ya Ashley Young, Marouane Fellaini, Juan Mata na Chris Smalling, hiyo ikiwa mara ya kwanza kushinda Man-City ugani Old Trafford.

Mwamuzi wa mechi ya leo atakuwa Andre Marriner mwenye umri wa miaka 48 ambaye amechezesha mechi tatu za Man-United msimu huu.