Wabunge David Ochieng', Mawathe waapishwa
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wapya waliochaguliwa majuzi katika chaguzi ndogo, David Ochieng (Ugenya) na Julius Mawathe (Embakasi Kusini) Jumanne waliapishwa bungeni ili kuanza kazi rasmi.
Waliapishwa na Karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai mbele ya Spika Justin Muturi.
Wawili hao waliibuka washindi katika chaguzi hizo zilizofanyika Aprili 5, 2019.
Bw Ochieng’ aliyewania kwa tiketi ya chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG), alimshinda mgombea wa ODM Chris Karan huku Bw Mawathe wa chama cha Wiper akimwonyesha kivumbi Irshad Sumra wa ODM.
Bw Karan alikuwa ameshinda kito cha Ugenya katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017, lakini Bw Ochieng’ akapinga ushindi huo mahakamani.
Kesi hiyo iliendelea hadi katika Mahama ya Juu iliyobatilisha ushindi wa Bw Karan kwa misingi kuwa ushindi wake haukuwa halali.
Naye Bw Mawathe alihifadhi kiti hicho alichokishinda katika uchaguzi mkuu wa 2017.
Kesi
Hii ni baada ya ushindi wake kufutuliwa mbali na mahakama katika kesi iliyowasilishwa na Bw Sumra.
Alipowasili bungeni Bw Ochieng alisindikizwa na Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi na kiranja wa wengi Benjamin Washiali.
Naye Bw Mawathe aliingia ukumbini huku akisindikizwa na Mbunge wa Kitui ya Kati, Makali Mulu na Bi Cecily Mbarire (Mbunge Maalumu).
Kulingana na kanuni za bunge, Bw Wandayi alimjulisha Bw Ochieng’ kabla ya kula kiapo huku Bw Mawathe alijulishwa kwa wabunge na Bw Mulu.
Badaye Spika Muturi aliwapa wawili hao, kila mmoja, nakala ya Katiba na Sheria za Bunge.