Makala

UVUMBUZI: Teknolojia mpya iliyoanza kwa Sh750 sasa humpa mamilioni

April 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na FRANCIS MUREITHI

UNAPOKUTANA naye kwa mara ya kwanza katika eneo la Pipeline kando ya mji wa Nakuru akipiga gumzo na wajenzi wanaojenga nyumba, utadhani yeye ni nyapara anayesimamia ujenzi huo.

Kumbe Bw James Mwangi ‘Kaka James’, 35, si nyapara bali ni mwekezaji chipukizi ambaye nyota yake inang’aa katika sekta hii ya ujenzi katika Kaunti ya Nakuru.

Bw Mwangi ameanzisha kampuni ya ujenzi ambayo inazingatia ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa kutumia matofali ya fungu-jenzi (blocks).

Safari yake ya ujenzi wa nyumba sampuli hii ilianza kama mzaha wakati aliponunua mfuko mmoja wa wa simiti miaka saba iliyopita na kuunda dirisha dogo la mawe ambalo hutumia kuingiza hewa safi kwenye nyumba.

Leo hii safari ambayo ilianza na Sh750, imwemwezesha kuweka jiwe la msingi la kampuni yake ijulikanayo kama Kaka James Construction Company ambayo inakadiriwa kuwa ya mamilioni ya pesa.

Aidha, kampuni hii imeweza kuwaajiri zaidi ya wafanyakazi 200 huku wengi wao wakiwa vijana barubaru kama yeye.

Bw Mwangi alipogundua kuwa biashara hii ina uwezo wa kupanuka katika siku za usoni, alikopa Sh50,000 kutoka kwa Hazina ya Vijana na kuanzisha kampuni hii.

Kaka James Concrete Enterprise inatumia teknolojia ya kuchanganya mchanga na simiti na kisha kuunda fungu-jenzi ili kutatua ukosefu wa nyumba za gharama ndogo kwa maelefu ya wakazi wa mjini Nakuru na vitongoji vyake.

Teknolojia hii ambayo inashika kasi na kuwavutia wakazi wengi imepunguza gharama ya ujenzi wa nyumba kwa kuwaondolea mahitaji mengi ambayo hufanya ujenzi wa nyumba kuwa wa gharama ya juu.

Fungu-jenzi hizi zinaundwa na mitambo ya kisasa aina ya hydraulic baada ya simiti na mchanga kuchanganywa vizuri kwa kipimo sawia.
Fungu-jenzi hizi zimewavutia wakazi wengi ambao wamezipigia debe kwani hazina adhari zozote kwa mazingira.

“Teknolojia hii ni ya gharama ya chini na wakazi wengi wa Nakuru wanaotamani kuishi kwa nyumba safi wanaweza kuitumia kujijengea makao safi ya kudumu na kupunguza ukosefu wa nyumba unaozidi kuongezeka mjini Nakuru na vitongoji vyake kutokana na ongezeko la watu ambao kufikia sasa ni zaidi ya milioni mbili,” anasema Bw Mwangi.

Aidha, Bw Mwangi anafichua kuwa teknologia hii yaweza kumaliza ukosefu wa nyumba na kuwapa afueni wakazi wa Nakuru wenye mapato ya chini kwani ujenzi wa nyumba hizo huchukua muda mfupi.

Teknolojia hii, anazidi kusema Bw Mwangi, ndiyo funguo za kutatua uosefu wa nyumba kwa wakazi wengi wanaoishi nyumba duni na wanasongwa na kodi inayozidi kuongezeka ya nyumba.

James Mwangi, mwanzilishi wa kampuni ya kuunda fungu-jenzi katika eneo la Pipeline, Nakuru. Picha/ Francis Mureithi

Na tangu aanzishe kampuni hii, wakazi wengi waliokuwa wamekataa tamaa ya kuishi kwenye nyumba zao na waliokuwa wanaishi nyumba za matope sasa wanatabasamu kwani wanaishi kwenye mazingira safi.

Aidha, amewekeza mamilioni ya pesa kwa kununua mitambo ya kisasa ya kuunda fungu-jenzi na kwa sasa yeye huunda takribani fungu-jenzi 2,000 kila siku na kuuza kati ya Sh60 na Sh70 kila fungu jenzi moja.

Bw Mwangi alipoanzisha biashara hii alipata faida ya Sh2,000. Hata hivyo, leo hii ana kila sababu ya kutabasamu kwani faida yake imeongezeka maradufu na hesabu yake ya kila mwaka hugonga Sh800,000.

“Fungu-jenzi hizi ni nyepesi na wakazi wengi wanaotaka kujenga nyumba za ghorofa huzinunua kwa wingi kwani zina mashimo maalumu amabo huruhusu hewa kuingia kwenye nyumba na kasha kutoka kwa urahisi,” anaeleza Bw Mwangi.

Uchoraji

Bw Mwangi ambaye alisomea Shule ya Msingi ya Hyrax na kisha kujiunga na Shule ya Upili ya Langalanga alipata mafunzo yake ya ujenzi katika chuo cha Kenya Industrial Training Institute (KITI) mjini Nakuru ambapo alihitimu kwa diploma ya uchoraji na kisha akajiongezea maarifa kwa kuhitimu katika ukaguzi wa hesabu katika Chuo Kikuu cha Egerton.

Mbali na kuunda fungu-jenzi, Bw Mwangi pia ni mtaalamu wa kuunda fungu-jenzi spesheli za kurembesha nje ya nyumba na njia fupi za kuingia kwenye nyumba.

“Wawekezaji wengi katika sekta ya ujenzi hupendela fungu jenzi hizi zenye mashimo wakati wa kujenga nyumba za ghorofa kwani hupunguza gharama ya ujenzi na muda unaotumiwa kukamilisha nyumba hizo,” anasema.

Wateja wake ni pamoja na shule,makanisa, wakazi wa kawaida, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge (CDF).

Je, nini siri ya kufaulu kwenye biashara hii katika kipindi kifupi cha miaka saba tu? Bw Mwangi anafichua kuwa siri ni kufanya kazi kwa bidii, kuwa mpole na kuwahudumia wateja wote bila kujali mapato yao.

“Bidii huleta kufaulu maishani na bidii yangu ndiyo msingi thabiti kwani lolote ninaloanzisha mimi huhakikisha linafaulu . Hali kadhalika mimi husikiza ushauri kutoka kwa watalamu na wafanyibiashara waliofaulu maishani,” anasema Bw Mwangi.

Mwekezaji huyu chipukizi anasema kuwa raha yake ni kuona wakazi wanaohangaika kujengea nyumba safi na za gharama ya chini wamefaulu.

Na bila shaka Bw Mwangi anaelewa umuhimu wa kuishi kwenye mazingira safi kwani alizaliwa kwenye kitongoji duni cha Wamagata katika eneo la Kiti ambapo wazazi wake walihangaika kulea jamii ya watoto wanane.

Bw Mwangi anasema kuwa gharama ya ujenzi wa nyumba yaweza kushuka kwa kiasi kikubwa ikiwa serikali itazingatia teknolojia hii.