Aliyeaga dunia ndani ya seli Maragua azikwa
Na MWANGI MUIRURI
HATIMAYE mwendazake Hamuel Muguro Ngugi aliyeaga dunia katika mazingara tata ndani ya kituo cha polisi cha Maragua, Kaunti ya Murang’a alizikwa Jumatano nyumbani kwao katika kijiji cha Gathigia/Irembu.
Hali ya majonzi ilitanda katika kijiji hicho huku waombolezaji wakiongea kwa hisia kuhusu ukatili wa kiutawala.
“Ukiwa maskini haki yako utaikosa hapa nchini… Alikamatwa bila hatia inayoeleweka, akazuiliwa katika mazingara hasi ikieleweka kuwa hakuwa
na buheri wa afya na hatimaye akaaga dunia bila wa kumsaidia asake matibabu,” akasema aliyezungumza kwa niaba ya marafiki zake, Peter
Njoroge.
Marehemu alikamatwa usiku wa Aprili 13, 2019, lakini akaaga dunia asubuhi iliyofuata akiwa ndani ya seli akingojea uamuzi wa ama aachiliwe au afunguliwe mashtaka.
Marehemu alikuwa mhudumu wa baa inayofahamika kama Starehe Bar katika mji wa Maragua kwa msingi kuwa akiwa na wenzake watatu walikuwa wakiuza pombe baada ya muda au saa inayokubalika kisheria.
Hata hivyo, uchunguzi umebainisha kuwa walikamatwa saa tano na dakika tano za usiku, muda wahudumu wa baa wanafaa wawe wakiandaa kufunga kazi baada ya uteja kutamatishwa kisheria saa tano usiku.
Bw Muguro alikamatwa akiwa pamoja na wenzake John Waithaka Njeri, Patrick Wairegi na Simon Kamari.
Baada ya Muguro kuaga dunia, maafisa katika kituo hicho ‘walimpeleka’ hadi hospitali kuu ya Maragua na ambapo maiti iliwekwa kwa Mochari ya
hospitali hiyo kabla ya kuhamishiwa katika ile ya Murang’a.
Tayari, mamlaka ya kuchunguza utendakazi wa maafisa wa polisi (IPOA) imetuma maafisa wake kuchunguza kisa hicho na ambapo mumiliki wa baa
hiyo Bw Amos Kinuthia ameelezea kuhusu uhasama uliokuwa kati yake na maafisa wa polisi na ambapo nia ilikuwa ya kumwadhibu kupitia msako
ndani ya baa hiyo.
Aidha, waliokuwa katika seli ya polisi pamoja na marehemu wameandikisha taarifa zao, huku tume ya kitaifa kuhusu ajira ya polisi
(NPSC) ikiongozwa na Bw Eliud Ndung’u Kinuthia ikitaka kuandaliwe ripoti ya kuelezea kama kuna aliyekuwa kwa lawama katika kizazaa hicho ili aadhibiwe ikiwa ni afisa wa polisi.
Marehemu Muguro alizaliwa mwaka wa 1973, akasoma hadi darasa la nne, akatoka kwao akaingia mtaani kujipa riziki, hapa na pale akajipata
kinyume na mkondo wa sheria na akafungwa gerezani miaka mitatu, waliozungumza kuhusu maisha yake ya uzimani wakasema alipenda pombe.
Mhubiri Samuel Kariuki wa kanisa la Deliverance la Kiamwamwangi, Kaunti ya Kiambu akiwa pia ni afisa wa polisi alisema vijana wengi wanafaa kuchukulia maisha kwa uzito unaofaa hasa katika safu ya kuanzisha familia zao.
Pia, kwa kuwa hakuna aliyetoa ushuhuda kuwa mwendazake alikuwa ametubu dhambi zake na kuokoka, mapasta waliokuweko waliwahamasisha
waombolezaji kuwa “ukiaga dunia bila wokovu wa kukutetea katika hukumu mbele ya kiti cha enzi, mambo yako huwa yameisha.”
Ilisemwa kuwa jinsi uagavyo dunia, ndivyo huwa umejitengea nafasi yako aidha katika afueni ya uzima wa milele au katika moto wa Jahanamu.
Aidha, Mhubiri Lukas Ndung’u ambaye aliongoza ibada ya mazishi alipinga vikali kuwa miaka ya kuaga dunia imewekwa kuwa 70 akisema kuwa kitabu cha Isaia 65:20 ndani ya Bibilia ya Wakiristo kimeweka miaka hiyo kuwa zaidi ya 100.
Pia, alipinga kuwa Mungu ana nafasi ya vijana na watoto katika hifadhi yake ya mauti, akisema kuwa “Biblia husema mbinguni kuna wazee 24 ambao wameripotiwa kuwa viongozi wa nyimbo za wasifu kuhusu Mungu, na hakuna mahali vijana au watoto hutajwa wakiwajibishwa majukumu katika ufalme huo.”
Akasema hilo lina maana kuwa mauti ya ujanani au utotoni huwa sio mapenzi ya Mungu na kuna haja ya watu wamnyenyekee ili awe akinusuru
vijana na watoto kutoka mauti.