TAJI LANUKIA: Manchester City sasa wanusa taji
MANCHESTER City walidumisha matumaini yao ya kuhifadhi ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kutia kapuni jumla ya mataji matatu msimu huu baada ya kucharaza Manchester United mabao 2-0 ugani Old Trafford mnamo Jumatano.
Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walishuka dimbani wakiwa na ulazima wa kusajili ushindi ili kuwaruka Liverpool kileleni mwa jedwali.
Ushindi kwa miamba hao wa soka ya Uingereza unawasaza na michuano mitatu pekee ili waweke historia ya kuwa kikosi cha pili baada ya Man-United kutetea kwa mafanikio ubingwa wa taji la EPL kwa misimu miwili mfululizo.
Man-City kwa sasa wanaselelea kileleni kwa alama 89, moja mbele ya Liverpool wanaonolewa na kocha Jurgen Klopp.
Tottenham Hotspur wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 70, tatu zaidi kuliko Chelsea watakaokuwa wageni wa Man-United wikendi hii uwanjani Old Trafford.
Arsenal waliokomolewa kwa mabao 3-1 na Wolves mnamo Jumatano uwanjani Molineux, wanakamata nafasi ya tano kwa alama 66, mbili mbele ya Man-United.
Baada ya Man-City kuambulia sare kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza wakicheza na watani wao wa tangu jadi jijini Manchester, vijana hao wa Guardiola walirejea ugani kwa matao ya juu na kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 54.
Nyota wa zamani wa AS Monaco, Bernardo Silva alishirikiana vilivyo na Raheem Sterling kabla ya kuvurumisha langoni kombora lililomzidi maarifa kipa David De Gea.
Mashihara ya beki Luke Shaw dakika 12 baadaye, yalimpa Leroy Sane nafasi ya kuwafungia waajiri wake bao lililodidimiza kabisa matumaini ya Man-United ya kutinga mduara wa nne-bora mwishoni mwa msimu huu.
Kulingana na Guardiola ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich, hatima ya Man-City katika kampeni za msimu huu imo mikononi mwao.
Ni matarajio yake kwamba ushindi dhidi ya Man-United utawapa masogora wake hamasa zaidi ya kuwakomoa Burnely mwishoni mwa wiki hii, siku mbili baada ya Liverpool kuchuana na Huddersfield ugani Anfield.
Kupimana ubabe
Baada ya kumenyana na Burnley, Man-City watavaana na Leicester City na Brighton ligini kabla ya kupimana ubabe na Watford katika fainali ya kuwania ubingwa wa Kombe la FA.
Kwa upande wao, Liverpool ambao wanafukuzia mataji mawili msimu huu, wameratibiwa kuchuana na Barcelona katika nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) hapo Mei 1 kabla ya kuwa wageni wa Newcastle United katika mechi ya EPL ugani St James Park.
Baada ya kurudiana na Barcelona uwanjani Anfield hapo Mei 7, Liverpool watapepetana na Wolves katika mechi ya mwisho ya EPL msimu huu.
Kwa upande wao, Tottenham watahakikisha wanamaliza kampeni za msimu huu katika nafasi ya tatu iwapo watawabamiza West Ham, Bournemouth na Everton katika mechi tatu zijazo.
Kikosi hicho cha kocha Mauricio Pochettino kinafukuzia pia ufalme wa UEFA na tayari kinapigiwa upatu wa kuwachabanga Ajax katika mikondo miwili ya nusu-fainali.
Akiwapa vijana wake malengo mapya, Guardiola amekitaka kikosi chake kuwa katili zaidi dhidi ya wapinzani wao katika mechi zilizosalia hasa ikizingatiwa kwamba Burnley waliwalazimishia Chelsea sare ya 2-2 mnamo Jumanne.