ANA KWA ANA: Apanga kuvunja kimya kwa albamu mwaka huu
ALIANZA kuimba akiwa ni mmojawapo wa wanachama wa kikundi cha Army G miaka kumi iliyopita na hata kurekodi albamu nzima, ‘Tumechange’.
Lakini miaka mitano iliyopita Antony Njoroge ‘Addeh Prince’ alikata shauri na kuanza safari kama mwanamuziki binafsi huku akizama kwenye mtindo wa reggae na Dancehall na kuangusha vibao kama vile What a friend, Feeling, No worry, U turn, na Set me free, alichozindua majuma matatu yaliyopita.
Lakini licha ya vibao hivi, maswali mengi yameibuka kuhusu mwendo wake wa kobe katika utunzi huku akitarajiwa kuzindua albamu yake ya kwanza mwisho wa mwaka 2019.
Ni miaka mitano sasa baada ya kuanza safari yako kama mwanamuziki binafsi, lakini hata albamu ya kwanza hauna. Kwa nini mwendo huu wa kobe?
ADDEH PRINCE: Nakubali kwamba kasi yangu kidogo iko chini. Lakini watu wanapaswa kuelewa kwamba ili kurekodi muziki wa ubora wa hali ya juu lazima uwekeze kitita kikubwa cha pesa. Wakati huo, ajira niliyokuwa nikifanya haingeniruhusu kuweka akiba ya pesa za usafiri, vile vile kurekodi audio na video za nyimbo.
Kwa hivyo albamu hii tuitarajie lini?
ADDEH PRINCE: Napanga kuizindua ifikapo Desemba mwaka huu.
Tufichulie machache kuihusu.
ADDEH PRINCE: Kwa sasa hilo litasalia kuwa siri. Nataka kuwashtua mashabiki wakati huo ukiwadia. Lakini kile ningeweza kusema ni kwamba albamu hiyo ya vibao kumi na tayari vibao viwili vimekamilika.
Set me free, kibao chako ulichozindua hivi majuzi kinaakisi hisia nyingi. Nini kilichochea utunzi wake?
ADDEH PRINCE: Kibao hiki kina umuhimu sana sio tu kwangu bali pia kwa familia yangu. Kinazungumzia matatizo maishani, uchungu wa kuwapoteza wazazi wote, na changamoto za kuinua taaluma yangu kimuziki, vile vile ya dadangu Nyce Wanjeri ambaye ni muigizaji.
Pole sana kwa kuwapoteza wazazi. Sasa kwa sababu umemtaja Nyce, aliyekuwa mojawapo ya washiriki wakuu katika kipindi cha Auntie Boss, hauhisi kana kwamba huenda ukatokomea katika maarufu wake?
ADDEH PRINCE: La hasha! Tunafanya kazi katika sekta tofauti. Aidha, sisi ni ndugu na tunatakiana mema. Hakuna ushindani wowote baina yetu na sijawahi kuwa na hisia za kutaka kushindania mwangaza naye. Isitoshe, ndugu yetu mdogo pia ni mwanarepa na anajitahidi kujiimarisha upande huo pasi kuwepo kwa nia ya kutaka kushindana nasi.
Ulianza vipi kazi ya usanifu mitindo?
ADDEH PRINCE: Nilianza kufanya kazi hii mwaka wa 2014 ambapo awali sikutambua kwamba ningeshamiri vyema katika fani hii. Tokea hapo penzi langu katika masuala ya fashoni limekuwa likinawiri. Najihusisha na mavazi kutoka nchini Italia huku nikishughulikia hasa wanaume. Ni jambo la kujivunia watu kutoka matabaka mbali mbali wanapokuja kwangu wakitaka huduma yangu.
Kuna watu maarufu ambao umekuwa ukiwavika?
ADDEH PRINCE: Naam, nimewahi kuhudumia wasanii kama vile Moji Short Baba, Ben Cyco, Two Comical Bigman miongoni mwa wengine wengi.
Unasawazisha vipi kuwa mwanamuziki na msanifu mitindo?
ADDEH PRINCE: Sio rahisi licha ya kuwa sekta hizi mbili zinaingiliana katika fani ya burudani. Ndiposa mwanzoni mwa mwaka huu niliamua kusitisha kidogo kazi ya usanifu mitindo, na badala yake kuangazia muziki.
Ulisomea IT chuoni lakini hukukamilisha. Kwa nini?
ADDEH PRINCE: Ukosefu wa pesa ndiyo ulichangia pakubwa uamuzi wangu wa kukatiza masomo chuoni. Nilikuwa najitahidi lakini pesa kidogo nilizokuwa nikiunda hazingetosha kulipa karo.
Tukirejea katika masuala ya muziki, kwa sasa nia yako ni kushirikiana na nani?
ADDEH PRINCE: Tangu jadi nimekuwa nikitamani kushirikiana na Dafari, na habari njema ni kwamba tunapanga kuangusha kibao hivi karibuni. Kimataifa ningependa kushirikiana na wasanii Sherwin Gardner kutoka Trinidad, vile vile Papa San, Christopher Martin na Romain Virgo kutoka Jamaica. Orodha ni ndefu siwezi wataja wote wanaopamba muziki wa reggae.
Christopher Martin na Romain Virgo? Wao sio mwanamuziki wa nyimbo za injili. Kama msanii wa injili hauhofii kushutumiwa kutokana na ushirikiano huu?
ADDEH PRINCE: Muziki wangu hasa ni wa ujumbe mzuri wa matumaini, na wasanii hawa wanafuzu. Isitoshe, midundo yao ni ya kuvutia.