'Miaka 60 ya kukupasha habari'
Na CHARLES WASONGA
FATAKI zilifyatuliwa angani katikati mwa jiji la Nairobi Ijumaa usiku pale Shirika la Habari la Nation (NMG) lilianzisha msururu wa sherehe za kuadhimisha miaka 60 tangu kuasisiwa kwake.
Kwa takriban dakiki 20 hivi milio na mwangaza wa fataki hizo zilihanikiza angani juu ya jumba la Nation Centre na kuwashtua baadhi ya watu waliokuwa wakiburudika katika vilabu vilivyoko kando ya barabara za Kimathi na Moi Avenue.
Wengine walidhani kuwa jumba na Nation Centre limevamiwa na magaidi lakini baadaye wakang’amua kuwa ilikuwa ni sherehe.
Licha ya hayo magari ya zima moto kutoka Serikali ya Kaunti ya Nairobi yalikuwa chonjo katika barabara ya Kimathi karibu na Nation Centre
kukabiliana na hatari zozote. Maafisa wa polisi na askari kadhaa wa kampuni ya ulinzi ya Seneca Security Guards Ltd walishika doria nje na ndani ya
jumba hilo kudhibiti umati wa watu na kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wasimamizi wa NMG Wilfred Kiboro na Afisa Mkuu Mtendaji Stephen Gitagama waliwaongozwa wanafanyakazi, wanachama wa wageni waalikwa katika sherehe hizo ambazo pia zilihusisha ukataji wa keki.
Mgeni mheshimwa katika sherehe hizo zilizofanyika katika eneo la kuwapokea wageni katika jengo la Nation Centre alikuwa Katiba wa Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Jerome Ochieng.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Balozi wa Ufaransa humu nchini Aline Kustermenager miongoni mwa wageni wengine.
Bw Kiboro alisema katika miongo hiyo sita NMG inajizatiti kutekeleza wajibu wake katika nyanja ya uanahabari, upaliliaji wa demokrasi, mtetezi wa
utawala wa kisheria na uchumi huria.
“Nguzo kuu ya katika utekelezaji wa wajibu wetu huwa ni kuzingatia ukweli, uhuru, haki, kutopendelea na uhalisi. Kampeni ya sasa dhidi ya ufisadi
inayoongozwa na mashirika ya habari ni kielelezo kuhusu namba vyombo vya habari vinaweza kuchangia mabadiliko ya kuboresha jamii na taifa kwa
jumla,” akasema.
Bw Kiboro aliahidi kwua NMG itasalia kutekeleza wajibu wake kwa njia huyo ili kukuza himaya na sifa yake kama mtetezi wa kweli wa haki za watu.
Sifa
Naye Bw Gitagama alilisifu shirika la NMG akilitaja kwa weledi wake katika kujuza, kufundisha, kuburudisha na kufichua maovu katika jamii kupitia
vyombo vyake kama vile magazeti, runinga, mtandao na hata redio.
“Ni fahari yetu kusimama na wanahabari wetu na hatuchelea kulinda maisha yao na kuhakikisha kuwa wanafanya kazi katika mazingira faafu,” akasema.
Hata hivyo, Bw Gitagama aliwashauri wanahabari wa NMG kuongozwa na uadilifu na uzingatia wa kanuni za kitaaluma katika utendakazi wao.
Alipoanzisha shirika hilo la habari miaka 60 iliyopita Mstahiki Aga Khan alikuwa akilenga kutoa jukwaa ambalo litatumiwa kuangazia na kuelezea stori za Waafrika kwa mtizamo wa Kenya.
Na chombo cha kwanza cha habari ambacho Aga Khan alianza nayo ilikuwa ni gazeti la Kiswahili la Taifa Leo mnamo 1959.
Gezeti hilo liliondokea kuenziwa zaidi na Waafrika enzi hizo kwani lilisheheni habari zilizohusu shughuli zao za kupambana na Ukoloni kando na masuala mengine ya kijamii.
Kampuni ya Habari ya Nation, kama ilivyojulikana wakati huo, ilipata umaarufu mkubwa kwa kupeperusha habari kuhusu uhuru wa Kenya mnamo 1963, mauaji ya wanasiasa mashuhuri kama vile Pio Gama Pinto (1965) na Tom Mboya (1969).
Vile Nation iliripoti kwa ufasaha katika magazeti yake ya Taifa Leo na Daily Nation matukio yote yaliyochangia kurejelea kwa mfumo wa utawala
wa vyama vingi nchini mnamo miaka ya 1980s na 1990s.
Leo hii NMG imeshamiri na kuanzisha vyombo vya habari katika mataifa ya Uganda, Tanzania na Rwanda.
Shughuli kadhaa zimeratiobiwa mwaka huu kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa shirika hili.
Shughuli hizo ni kama vile za kishirikisha na kuwatuza wafanyakazi, maonyesho ya kazi za sanaa na picha, kuwatambua na kuwatuza wateja, wauzaji
magazeti, wasambazaji na kufurahia turathi za Jiji la Nairobi kupia mashindoni ya Riadha na fani nyinginezo za kijamii zinazolenga elimu.