Makala

OBARA: Usajili wa Huduma Namba umefichua ‘Kenya mbili'

April 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

WAKATI wowote unaposikia mtu akisema Kenya imegawanyika, jambo la kwanza ambalo kwa kawaida huja akilini mwa wengi wetu ni kuhusu mgawanyiko wa kikabila au kisiasa.

Kwa kiwango fulani, mgawanyiko huu unaweza kuwa wa kidini au kati ya walio maskini na matajiri katika jamii.

Lakini katika siku za hivi majuzi, nimegundua Kenya ina mgawanyiko wa hali nyingine ya kipekee. Hii inahusu waraibu wa kutumia mitandao ya kijamii, na wale ambao hawategemei sana teknolojia hizo za kisasa za mawasiliano kwa shughuli zao za kila siku.

Nikiwa katika pilkapilka zangu za kawaida mitaani, mashambani na vile vile nilipokuwa nikipekuapekua mitandao tofauti ya kijamii, nilibaini Wakenya wana misimamo tofauti mno kuhusu usajili wa Huduma Namba unaoendelezwa na serikali kuu.

Upande mmoja kuna raia ambao wanapinga shughuli hii, wakidai kuhofia jinsi haijulikani kama habari za kibinafsi kuwahusu zinazokusanywa na serikali zitahifadhiwa kwa njia salama ambayo haitawahatarishia maisha yao.

Kwa upande mwingine, kuna wananchi wanaomiminika kwa wingi katika vituo vya usajili wa Huduma Namba mitaani, mijini na mashambani.

Nimeshuhudia watu wakitoka maeneo ya miji mikubwa na kuekekea viungani mwa miji hiyo kujisajili kwani kule wanakoishi kuna foleni ndefu kila wakati.

Pia nimeona wakazi wa mijini wanaokuta vituo bila watu wengi wanapoenda mashambani wakitumia fursa hiyo kujisajili kwa haraka.

Kile kinachojitokeza ni kuwa kwa mtazamo wangu, idadi kubwa ya watu wanaojisajili kupokea Huduma Namba ni watu ambao siogopi kusema hawana uraibu mkubwa wa kutumia mitandao ya kijamii.

Hawa ni wananchi ambao hushawishika zaidi kwa habari wanazopokea kutoka kwa vyombo vya kidesturi kama vile redio, televisheni na magazeti na pia kutoka vinywani mwa viongozi wenye ushawishi kama vile wanasiasa, viongozi wa kidini na maafisa wa serikali wakiwemo machifu.

Wananchi hawa wameitikia wito wa kujisajili licha ya pingamizi kali inayoenea kwenye mitandao ya kijamii na vile vile kesi iliyowasilishwa mahakamani kutaka usajili huo usitishwe. Itakumbukwa kesi hii ilifanya korti iagize serikali isilazimishe mtu yeyote kujisajili.

Ninachoshuhudia hapa ni kwamba kuna Kenya mbili. Ya mtandaoni, na ya hali halisi ya kimaisha. Hii ni hali ambayo tumewahi kuona awali katika siasa hasa ifikapo wakati wa uchaguzi, ambapo utakuta Wakenya mitandaoni wakimshabikia sana kiongozi fulani lakini kura zinapohesabiwa anaweza hata kuzirahi kwa vile hali halisi huwa tofauti kabisa.

Tafiti mbalimbali huonyesha Kenya ni miongoni mwa mataifa Afrika yanayoongoza kwa utumizi wa mitandao ya kijamii na hii inasemekana inaweza kutumiwa kuleta mabadiliko makubwa katika jamii kama vile kuimarisha uongozi bora.

Ingawa tumeona mara kadhaa Wakenya wakiungana mitandaoni kupigania mambo mbalimbali hadi yatimizwe, mabadiliko makubwa katika jamii hayatatokea kupitia kwa mitandao hii kama pengo lililopo kati ya waraibu na jamii halisia halitazibwa!