Michezo

Ingwe wakataa kurudia mechi dhidi ya Sony Sugar

April 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN ASHIHUNDU

Wasimamizi wa klabu ya Ingwe wamepinga uamuzi wa KPL kuamuru mechi yao iliyotibuka dhidi ya Sony mnamo April 14 irudiwe katika uwanja wa Awendo mnamo Mei 12, siku chache tu kabla ya mabingwa hao mara 13 kukutana na mahasimu wao, Gor Mahia.

Mechi hiyo ya Ligi Kuu ya SportPesa ilitibuka kufuatia mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo na wasimamizi wakaamua irudiwe siku iliyofuata, lakini pia haikuchezwa baada ya Leopards kukataa wakidai wenyeji Sony hawakutimiza masharti ya ligi.

Wakipinga umuzi huo, Leopards walisema hawakusababisha kutibuka kwa mechi hiyo, na kamwe hawatafunga safari ya kilomita 400 kurudi Awendo kucheza mechi hiyo.

“Tutakubala tu kucheza iwapo mechi hiyo itahamishwa Kisumu au Nakuru,” katibu wa Leopards Oscar Igaida alisema.

Lakini kocha wa Sony Sugar, Patrick Odhiambo aliwashutumu Leopards kwa kubuni vijisababu vya kuwafanya wakose kuicheza mechi hiyo.

Mechi ya Awendo ilitibuka dakika ya 68 wakati Leopards walikuwa wakiongoza kwa 1-0, bao lililofungwa na Whyvonne Isuza.