ODONGO: Wanasiasa wa Homa Bay wakomeshe malumbano
Na CECIL ODONGO
MALUMBANO yanayoshuhudiwa kati ya wanasiasa wa Gatuzi la Homa Bay kuhusu kiti cha ugavana yanatia breki wajibu muhimu wa viongozi kutekeleza miradi ya maendeleo kwa raia waliowachagua.
Utata mkubwa ambao umezua makundi mawili pinzani unahusu uwezo wa Gavana Cyprian Awiti kuongoza baada ya kutoonekana hadharani kwa muda mrefu, duru zikiarifu amekuwa akitibiwa nchini Ujerumani japo amesharejea nchini.
Kundi linaloongozwa na Seneta Moses Kajwang, Mbunge wa Homabay Mjini Peter Kaluma na madiwani kadhaa limejitokeza hadharani na kumtaka Bw Awiti ajiuzulu wadhifa huo kutokana na matatizo ya kiafya yanayomkabili.
Wawili hao pia wametaja kutoridhishwa na jinsi Naibu Gavana Hamilton Orata amekuwa akiendesha shughuli za kaunti, likisema hakuna miradi yoyote ya maendeleo inayotekelezwa huku sekta za matibabu, maji na kilimo zikiendelea kudorora.
Kundi jingine linaloongozwa na Mbunge wa Suba Kusini John Mbadi na washirika wa Gavana hata hivyo limelaumu kambi ya Mabw Kajwang na Kaluma kuwa kuzua taharuki na kuwachochea wakazi dhidi ya kaunti.
Bw Mbadi anadai kwamba hata Bw Awiti akijiuzulu, serikali ya kaunti itaendeshwa na Bw Orata ambaye anapigwa vita na kundi pinzani na akawataka Mabw Kajwang na Kaluma kusubiri hadi mwaka wa 2022 ili kupambana naye kuwania kiti cha ugavana.
Bw Awiti naye ameeleza kutofurahishwa kwake na jinsi kundi la seneta huyo limekuwa likimpiga vita, akisema wawili hao hawajafaidi wakazi wa Homabay kivyovyote licha ya kuhudumu katika nyadhifa zao kwa miaka mingi. Ingawa hivyo, makundi haya mawili yanafaa kukomesha makabiliano na kuungana ili kuwanufaisha wananchi.
Inashangaza kwamba Bw Mbadi, anayeshikilia wadhifa wa hadhi wa Kiongozi wa Wachache kwenye bunge la taifa ana uwezo wa kuwafikia wawekezaji na hata Rais Uhuru Kenyatta kuomba serikali izindue na kutekeleza miradi ya maendeleo Homabay, anajishughulisha na siasa za mashinani bila kueleza alichotendea watu wa eneobunge lake.
Seneta Kajwang’ naye anafaa kuweka serikali ya kaunti mizani na kufuatilia jinsi fedha zinavyotumika badala ya kushiriki siasa za kujipigia debe akilenga wadhifa wa ugavana.
Bw Kaluma anafaa kuwa mtu wa mwisho kukashifu kaunti kuhusu miradi ya maendeleo ilhali eneobunge lake limewahi kutajwa kati ya maeneo yasiyotumia vizuri fedha kutoka kwa Hazina ya eneobunge hilo(CDF).
Hata hivyo, Gavana pia hafai kujibizana na wanasiasa hawa na badala yake awahudumie wananchi kwa kutekeleza ahadi alizotoa akisaka kura. Ni jambo lisilopingika kwamba Homabay haijivunii kukamilika kwa mradi wowote wa maana tangu Bw Awiti aingie mamlakani 2013.
Kwa kweli Homabay haijakuwa na utulivu tangu uchaguzi wa mwaka wa 2017 kutokana na kesi ya kupinga uchaguzi wa gavana na pia ni kati ya kaunti ambazo zipo nyuma kimaendeleo licha kwamba ni kitovu cha siasa za Luo Nyanza.
Cha muhimu kwa sasa ni Gavana, Seneta, Wabunge na Wawakilishi wadi kuungana na kuwahudumia raia kwa miaka mitatu iliyosalia kisha kutumia huduma hizo kama msingi wa kujivumisha kwa raia 2022.