• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
ADUNGO: Kiini cha tofauti za matumizi ya lugha katika miktadha mbalimbali

ADUNGO: Kiini cha tofauti za matumizi ya lugha katika miktadha mbalimbali

NA CHRIS ADUNGO

MATUMIZI ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika (King’ei, 2010).

Muktadha wa mazungumzo ni hali au mahali ambapo mazungumzo yanafanyika. Katika muktadha wa mazungumzo, kuna mambo ambayo huathiri matumizi ya lugha na kusababisha tofauti za matumizi ya lugha katika muktadha mmoja hadi mwingine.

Matumizi ya lugha katika muktadha wa mazungumzo huathiriwa na mambo makuu matatu: (i) mada ya mazungumzo, (ii) uhusiano wa wazungumzaji, na (iii) mahali pa mazungumzo. Kwa ujumla, matumizi ya lugha kwa kuzingatia muktadha wa mazungumzo, huzaa mitindo tofauti ya uzungumzaji ndani ya jamii-lugha inayohusika.

Matumizi ya lugha ni dhana pana kwa maana kwamba imebeba mawasiliano ya wanajamii. Mawasiliano hayo yanaweza kuwa katika muktadha wa mazungumzo au maandishi (Msanjila na wenzake, 2011).

Kwa mujibu wa King’ei (2010), muktadha ni ile hali inayotawala na kuelekeza matumizi ya lugha inayozungumzwa, kwa mfano, mahali, wakati, hadhira, kusudio la msemaji nk.

Kadhalika, katika lugha ya mazungumzo, wazungumzaji wengi hushawishika kutumia aina fulani ya lugha kulingana na muktadha fulani ambao hutofautiana na muktadha mwingine.

Hali hii inaonyesha kuwa kuna mambo fulani ambayo huwafanya wazungumzaji wa lugha wateue msamiati fulani katika mazungumzo yao unaolingana na muktadha walipo wakati huo. Mada, uhusiano na mahali ni mambo makuu matatu yanayozingatiwa na wazungumzaji wanapotumia lugha katika miktadha mbalimbali ya mazungumzo.

Katika miktadha tofauti ya mazungumzo kwa kiasi kikubwa, matumizi ya lugha hutegemea wazungumzaji wa lugha hiyo wanavyoz- ingatia kaida za mazungumzo kulingana na muktadha unaohusika (Masebo na Nyang-? wine, 2004). Matumizi ya lugha katika muktadha wa mazungumzo kama dhana, huchambuliwa na kufafanuliwa kwa namna tatu.

Kwanza, ni kwa namna ambavyo wazungumzaji wa lugha huitumia lugha yao kwa kuzingatia mada inayowasilishwa katika mazungumzo yanayohusika.

Pili, ni kwa jinsi ambavyo wazungumzaji wa lugha huitumia lugha kwa kuzingatia uhusiano baina ya wazungumzaji wa matabaka au makundi tofauti.

Tatu, huchambuliwa kwa namna ambavyo wazungumzaji wa lugha huitumia lugha kwa kuzingatia mahali ambapo mazungumzo hayo yanafanyika (Msanjila na wenzake, 2011). Msingi wa lugha ya mazungumzo unatokana na wazungumzaji wenyewe wa lugha wanavyoitumia lugha yao.

Kwa kawaida, wazungumzaji wa lugha huitumia lugha yao kwa kuzingatia kanuni na kaida za mazungumzo ambazo hutawala kwa mujibu wa taratibu, mila na desturi za jamii inayohusika.

Kwa mfano, mtoto anapozungumza na mzazi wake, huteua maneno yanayoonyesha utii kwa mzazi huyo, na huacha maneno ya mtaani (vijiweni) ambayo anaweza kuyatumia anapozungumza na watoto wa rika lake.

Kwa hakika, hapo uhusiano baina ya mzungumzaji na msikilizaji hutawala na kuathiri mazungumzo baina ya wahusika wa mazungumzo. Katika kuielewa lugha ya jamii yoyote iwayo kunafungamana na kuielewa vyema jamii yenyewe ikiwa ni pamoja na kuyaelewa matabaka na makundi mbalimbali yaliyomo katika jamii hiyo.

Kwa mujibu wa Msanjila na wenzake (2011) jamii huundwa na matabaka na makundi mbalimbali ya watu.

Kwa mfano, kuna matabaka ya watawala na watawaliwa, wakulima na wasio wakulima, wafanyakazi wa kuajiriwa na wasio wa kuajiriwa, waliosoma na wasiosoma, wafanyabiashara na wasio wafanyabiashara nk.

Pia, kuna makundi ya vijana, wazee, wanawake, wanaume, wanafunzi, wanachuo, wanamichezo, wanajeshi, walimu nk.? Tukichunguza kwa makini, tutaona kuwa kila tabaka au kundi fulani la watu katika jamii linatumia aina fulani ya lugha inayoelekea kufanana, ambayo pia hulitofautisha tabaka au kundi moja na jingine katika jamii hiyo.

Tunapochunguza matumizi ya lugha katika miktadha mbalimbali, wakati mwingine tunaweza kujiuliza swali; kuna umuhimu gani wa kuchunguza na kufafanua tofauti za matumizi ya lugha katika miktadha mbalimbali ya mazungumzo?

Kwa mujibu wa Msanjila na wenzake (2011) kuchunguza na kufafanua tofauti za matumizi ya lugha katika miktadha mbalimbali ya mazungumzo kuna umuhimu wa aina tatu.

Kwanza, kunawasaidia watumiaji wa lugha kujua lugha ipi watumie katika miktadha rasmi na isiyo rasmi wanayozungumza wanajamii wenyewe.

Pili, kunawasaidia wazungumzaji wa lugha kuelewa namna bora ya kutumia lugha katika mawasiliano ya jamii baina ya mzungumzaji na msikilizaji.

Tatu, kunawasaidia watumiaji wa lugha, hususan kwa watumiaji wageni wa lugha kuelewa namna ya kuitumia vizuri lugha ya jamii ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni na kaida za mazungumzo na uteuzi sahihi wa maneno. Kwa mfano, kwa kuzingatia kaida na kanuni za mazungumzo, mzungumzaji mzee hataweza kutumia lugha ya vijana kwa kuzungumza na wazee wenzake (Hymes, 1964).

Badala yake, atajibidiisha kutumia lugha inayokubalika na wazee wa rika lake katika jamii inayohusika.

You can share this post!

KAULI YA WALIBORA: Tulitafune hili fupa ‘etimolojia’

ADA YA UJENZI: Atwoli atasaliti wafanyakazi?

adminleo