AKILIMALI: Kilimo cha mchele ndicho natija Kirinyaga
Na CHRIS ADUNGO
KWA miaka mingi sasa, wakulima wamekuwa wakitia bidii katika masuala ya kilimo kwa nia ya kujipatia faida nyingi.
Mbinu tofauti zimetumika kukiboresha kilimo tangu ujio wa sayansi na teknolojia mbalimbali huku mabilioni ya pesa yakiwekezwa na serikali na watu binafsi ili kusaidia mkulima wa kawaida kunufaika kwa mbegu, mbolea na pembejeo nyinginezo.
Hapa nchini, kilimo cha mchele huwa kinafanyika kwa wingi katika kaunti mbili pekee: Kirinyaga na Kisumu. Kaika Kaunti ya Kirinyaga na haswa eneobunge la Mwea, mchele hukuzwa kwa wingi huku eneo hili likitoa asilimia 80 ya mchele unaokuzwa nchini.
Mchele unaokuzwa kwa wingi hapa ni wa aina ya Pishori. Katika eneo la Nyangati, Kaunti ya Kirinyaga, Jarida la Akilimali lilikutana na Bw Samwel Muchiri mwenye umri wa makamo na ambaye ni mkulima wa mchele kwa miaka minane sasa.
Ziadi ya mchele, pia anakuza ndizi na viazi vitamu. Bw Muchiri anasema kwa sasa ana tajriba ya kutosha katika ukulima huu kwani miaka hii yote ameweza kujifunza mengi.
Kwa kawaida, huwa analima kwa misimu miwili huku msimu wa kwanza ukiwa kati ya mwezi wa nane hadi Disemba na msimu wa pili ukiwa kati ya mwezi wa kwanza hadi wa nne.
Shughuli hizi zinapoanza, huwa anatayarisha shamba lake kwa kulijaza maji kwani mpunga huhitaji maji kwa wingi haswa wakati wa kupanda.
“Kando ya shamba katika kijisehemu kidogo, huwa natayarisha mbegu za mpunga kwa kuzipanda ili kuzipa nafasi ya kukua na kuwa miche na baada ya wiki tatu huwa naihamisha na kuipanda katika sehemu nyinginezo za shamba,” anadokeza Bw Muchiri.
Anapopanda, maji huhitajika kufurika na baada ya siku tatu hivi anayapunguza ili kuwezesha miche hii
kukua na kunawiri vizuri. Wakati huu, pia huwa anatumia mbolea na baada ya wiki tatu, anaanza kupalilia
kwa kutoa majani, magugu na mimea inayokua na isiyohitajika. Zoezi hili huwa linafanyika kwa mikono na kwa kawaida, huwa anajiri wafanyakazi sita wamsaidie kwa shughuli hizi za upanzi.
Kulingana naye, huwa anaongezea mbolea mimea hii inapofikisha miezi mitatu na kisha kunyunyizia dawa ya kupigana na wadudu. Mmea huu unapofika mwezi wa nne baada ya upanzi kufanyika, huwa unaanza kutoa mazao na wakati huu ndege huanza kuuvamia.
Hivyo basi, kwa mwezi mmoja hivi, huwa inambidi kuwa makini sana kuwafurusha na kuwawinga ndege hawa kila mara wanapoingia shambani kutoka asubuhi hadi jioni.
Wakati huu, sasa maji huwa yamezuiwa kuingia shambani ili kuupa mpunga nafasi mwafaka ya kukua na
Kukomaa kuwa mchele. Mwishoni mwa mwezi wa wa nne, huwa anavuna na kuyaweka mazao kwenye ghala kusubiri wakati mwafaka wa kuuzwa kwa mazao.
Kwa kawaida, huwa anafanya kilimo hiki shambani mwake katika sehemu ya robo ekari na nusu ekari
ambapo huwa ana uwezo wa kuvuna kati ya gunia 10-20.
Kulingana naye, kilimo ni shughuli ambayo humpa riziki ya kila siku kwa kuilisha familia yake kwa kuwa hii ndiyo ajira yake ambayo anaitegemea pakubwa. Bw Muchiri anaelezea kuwa kilimo hiki hata hivyo kina changamoto kwani misimu mingine yenye kiangazi
husababisha upungufu wa maji na hili husababisha mchele kuvamiwa na wadudu. Wadudu hawa wanapovamia, hupunguza kiwango cha mavuno na tena dawa za kuwaondoa kwa kawaida huwa ni za bei ghali.