Michezo

Mashabiki wataka uwanja wa Afraha ufungwe ili ukarabatiwe

May 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MAOSI

UWANJA wa Afraha mjini Nakuru bado uko katika hali duni kutokana na utepetevu wa mwanakandarasi aliyesitisha ukarabati.

Sehemu ya mashabiki, uga wa kufanyia mazoezi, vyumba vya kubadilishia nguo na usalama kwa jumla ni baadhi ya mambo yaliyopuuzwa kwa muda mrefu.

Wakati mmoja mashabiki walilaumiwa kwa kuchangia uharibifu wake kwa mizozo ya mara kwa mara baada ya mechi.

Jambo hili limekuwa likiachia timu mzigo mzito wa kugharamia ukarabati, kwa mujibu wa kanuni ya usimamizi wa uwanja.

“Uwanja ubakie katika hali nzuri, la sivyo timu italazimika kubeba msalaba kwa niaba ya mashabiki,” mmkufunzi mmoja ambaye hakutaka kutajwa alisema.

Uwanja wa Afraha miaka ya hivi karibuni, umekuwa ukiandaa sikukuu za kitaifa kama vile Leba Dei, Jamhuri na Mashujaa.

Pia makao rasmi kwa timu za nyumbani yaani Ulinzi Stars inayoshiriki ligi kuu, St Joseph FC (supa ligi) na Nakuru All Stars (ligi ya daraja la pili).

Mnamo 2018 gavana wa Nakuru Mheshimiwa Lee Kinyanjui, aliahidi kuweka mikakati ya kuboresha miundo mbinu pamoja na kuleta vifaa vya kisasa.

Lakini bado ahadi haijatimia kwani bado viti vimetengenezwa kwa mbao na vimevunjikavunjika.

Barabara ya kuingia uwanjani haina lami na hakuna sehemu rasmi ya wageni kutulia wakashuhudia michuano.

Walevi na wezi wamekuwa wakihangaisha mashabiki kwa kuwaibia simu na kuleta usumbufu wa kila aina.

Hili linachangiwa na sehemu ya nyuma iliyo wazi, inayowaruhusu mashabiki kuruka ua na kuingia uwanjani wakati wa michuano.

Silas Alumasa shabiki wa timu ya Ulinzi anasema serikali inafaa kutoa agizo la kufungwa kwa viwanja vibovu vya ligi kuu.

“Ili kutoa muda kwa ukarabati visije vikahatarisha maisha ya mashabiki na vyumba vya kubadilishia nguo viwe vya hadhi nzuri, vifungwe,”alisema.

Anasema mingi ya miradi aliyoahidi Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Rutto wakati wa kampeni za uchaguzi 2017 imebaki kuwa hewa.

Afraha inaweza kubeba mashabiki 8,200 kwa wakati mmoja, lakini hali yake mbaya inaweza kupunguza kiwango hicho hadi 4000 hivi.

Kwa upande mmoja mashabiki wanaendelea kunyooshea tume ya michezo katika kaunti kidole cha lawama kwa kutowajibika ili kurekebisha baadhi ya sehemu.

“Ni jambo la kutia aibu kuona uwanja wa hadhi kuezekwa kwa mabati yaliyochakaa,” aliongezea.

Msimamizi wa shuguli katika uwanja wa Afraha ambaye hakutaka kutajwa jina lake anasema mwanakandarasi alisimamisha ukarabati ghafla.

Alieleza kuwa ukuta haukupakwa rangi wala kufikia kina kinachohitajika cha zaidi ya mita nane.

“Ndio sababu vijana kutoka kwenye mitaa jirani ya Bondeni na Kivumbini hupata muda rahisi wa kuvuka ukuta na kuiba mali ya uwanja,” alisema.

Alisema polisi wamekuwa wakishika doria tu wakati wa mechi ili kuzuia vurugu lakini wakati mwingi vijana wamekuwa wakitumia fursa ya ukosefu wa usalama kuharibu mali.

Aidha anawalaumu mashabiki wakati mwingine ,wanapokosa kudhibiti hisia zao pale wanapoanza kupigana na kuharibu mali.

Ndio sababu washika dau walibuni katiba inayoachia wasimamizi wa timu gharama ya kukarabati uwanja endapo timu zao zingechangia uharibifu wa uwanja kwa njia moja au nyingine.

Baadhi ya wakufunzi wanasema vyumba vya kubadilisha nguo, maji safi na usalama ni miongoni mwa masaibu wanayopitia wachezaji wakifika katika uwanja wa Afraha.