• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
DAU LA MAISHA: Amejitolea kuwapa wasichana visodo

DAU LA MAISHA: Amejitolea kuwapa wasichana visodo

NA PAULINE ONGAJI

Tafiti kadha zimeonyesha kwamba wakilinganishwa na wavulana, wasichana wengi nchini hukosa kwenda shuleni mara nyingi kwa ukosefu wa visodo.

Hii ni mojawapo ya sababu ambazo zimemsukuma Everlyne Bowa, 28, kujipa jukumu la kuwasaidia wasichana wa eneo la Olympic, kitongoji duni cha Kibra kupata bidhaa hii muhimu.

Ni shughuli ambayo amekuwa akiifanya kwa mwaka mmoja unusu sasa. Kinachofanya jitihada zake kuwa spesheli ni kwamba anajifadhili yeye mwenyewe.

“Mimi huunda begi maalum za mitindo ya Kiafrika ambapo faida ninayopata kutokana na biashara hii hunisaidia kufadhili mradi huu. Aidha, napata mafunzo ya ajira(internship) kutoka shirika moja nchini, ambapo malipo ninayopokea, pia hunisaidia kuendeleza shughuli hii,” aeleza Bi Bowa ambaye pia anasomea Ustawi wa kijamii katika Chuo Kikuu cha Daystar.

Kwa mwezi, Bi Bowa hutumia Sh10,000 kununua visodo huku akishirikiana na shule tano kutoka eneo hili kuzigawa. Kufikia sasa amefanya kazi na shule mbalimbali ikiwa ni pamoja na Sturgeon Academy, Miracle and Victory, Ayani Estate Primary School, Toi Primary School na Hope Academy ambapo kwa kila shule wasichana 30 hunufaika.

“Kila mwezi jumla ya wasichana 150 hufaidika kutokana na visodo hivi. Japo huenda watu wakadhani kwamba idadi hii ya wasichana wanaonufaika ni ndogo, hiyo ndio tunaweza kumudu kifedha kwa sasa,” aeleza.

Anasema kwamba wasichana wanaofaidika ni wale ambao wako katika darasa la nane wanaojiandaa kufanya mtihani wao wa kitaifa. Kati ya hawa, pia kuna mambo wanayoangalia kabla ya msichana kufuzu kupokea msaada huu.

“Hasa tunawaangazia wale walio na virusi vya HIV au wanafanya vibaya kimasomo. Pia, kuna wale wanaotoka katika familia maskini ambapo mara nyingi walimu hutusaidia kujua nani hasa anayehitaji msaada zaidi,” asema.

Mchango wake unazidi kuhisiwa kwani mradi huu umeimarisha matokeo ya wanafunzi wengi ambao awali waliathirika na tatizo hili.

“Pia, kuna wale ambao hawakuwa wanakamilisha kazi zao za ziada lakini kwa sasa wanafanya vyema. Aidha, usafi umeimarika miongoni mwa waliokuwa wameathirika, huku wale ambao kidogo walikuwa hawajiamini, wakionyesha ukakamavu hasa kwa kuchangia kila tunapoandaa vikao shuleni mwao,” aongeza.

Ni shughuli ambazo zimemfanya Bi Bowa kutambuliwa hasa katika mtaa huu. “Nimetambuliwa na chifu, vile vile viongozi wengine wa eneo hili. Pia, mara kadha wa kadha wazazi wa watoto wanaonufaika wamekuwa wakija kunishukuru kwa kazi ninayofanya,” aongeza.

Ari ya kujihusisha na shughuli za ugawaji visodo ilitokana na maisha magumu aliyopitia ili kupata bidhaa hii alipokuwa shuleni.

“Watu hudhani kwamba ukiwa na wazazi basi ni rahisi kupata bidhaa hii unapoanza kushuhudia hedhi. Kwangu haikuwa hivyo kwani kwanza kabisa utamaduni wetu haungeruhusu wazazi wangu kunizungumzia kuhusu masuala ya uzazi. Hii inamaanisha kwamba niliposhuhudia hedhi kwa mara ya kwanza ilikuwa vigumu kwangu kuwaendea wazazi, suala lililonifanya kutumia soksi kwa mwaka mmoja unusu. Pia, wazazi wangu walikuwa maskini na hivyo kulikuwa na changamoto ya kifedha,” aeleza.

Hili lilimuathiri kimasomo kiasi kwamba matokeo yake shuleni hayakuwa mazuri. “Hii ni mojawapo ya sababu iliyonifanya kujumuisha kikundi cha wasichana wasiofanya vyema shuleni kunufaika na mradi huu,” asema.

Kwa sasa mpango wake mkuu ni kuanzisha mradi wa kuunda visodo vinavyoweza kurudiwa. “Tayari nimeshafunza kikundi cha wasichana 20, ambapo kufikia mwezi Agosti tunatarajia kuanzisha rasmi shughuli hizi endapo tutakuwa na usaidizi wa kifedha,” aeleza.

Pia, matumaini yake ni kueneza mradi huu katika vitongoji duni vingine jijini na nchini ambapo analenga mitaa ya Dandora, Kawangware na Eastleigh.

You can share this post!

Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kufunguliwa Agosti

Wabunge waongezewe mishahara, Wakenya wamewageuza benki...

adminleo