Arsenal sasa macho yote kwa Europa League
ARSENAL wamehimizwa na kocha wao Unai Emery kuelekeza macho na makini yote kwa kampeni za Ligi ya Uropa baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Brighton wikendi jana kuzima ndoto zao za kumaliza kivumbi cha EPL muhula huu ndani ya mduara wa nne-bora.
Arsenal wanapigiwa upatu wa kukutana na Chelsea katika fainali ya Ligi ya Uropa baada ya kuwapepeta Valencia 3-1 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali wiki jana.
Chelsea ambao wamejipa uhakika wa kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao, walilazimishiwa sare ya 1-1 na Eintracht Frankfurt ya Ujerumani katika nusu-fainali ya Ligi ya Uropa ugenini.
Hadi kufikia walipo kwa sasa katika Ligi ya Uropa, Arsenal walipita mtihani mgumu wa Napoli katika hatua ya nane-bora ili kujikatia tiketi ya kuchuana na Valencia ambao ni miongoni mwa miamba wa soka nchini Uhispania.
Katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali, Arsenal waliwapepeta Napoli 2-0 uwanjani Emirates kabla ya kuwapokeza kichapo cha 1-0 nchini Italia.
Kwa upande wao, Chelsea waliwakomoa Slavia Prague kutoka Jamhuri ya Czech kirahisi kabla ya kukutana na Frankfurt waliowazidi ujanja Benfica kutoka Ureno.
Chini ya kocha Maurizio Sarri, Chelsea waliwachabanga Arsenal 3-2 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa kampeni za EPL mnamo Agosti 2018.
Hata hivyo, mkufunzi Unai Emery ambaye pia huu ni msimu wake wa kwanza katika soka ya Uingereza, aliwaongoza Arsenal kulipiza kisasi katika mchuano wa mkondo wa pili ligini humo.
Kwingineko, kocha Pep Guardiola wa Manchester City amekiri kwamba kipute cha kuwania ubingwa wa soka ya Uingereza (EPL) ndicho kigumu zaidi miongoni mwa Ligi Kuu tano za bara Ulaya.
Hadi alipotua kambini mwa Man-City mnamo 2016, Guardiola alikuwa amenyanyua mataji yasiyo idadi katika kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na soka ya Ujerumani (Bundesliga).
Akihojiwa na wanahabari kabla ya kuwaongoza vijana wake kuchuana na Leicester City mnamo Jumatatu usiku ambapo City walishinda 1-0 katika kivumbi cha EPL ugani Etihad, Guardiola alisema kwamba viwango vya ushindani katika soka ya Uingereza ni vya ‘kutisha’.
Man-City na Liverpool wamekuwa na msimu ambao umetawaliwa na ushindani mkali, huku wawili hao wakibadilishana usukani wa jedwali kwa mara 35.
Aidha, alama zinazojivuniwa na vikosi hivyo kwa sasa ni za juu zaidi kuliko ambazo zimewahi kuvunwa na mabingwa mara 13 wa taji hilo, Manchester United katika historia ya kampeni zao.
Man-City ambao pia wanafukuzia ubingwa wa Kombe la FA msimu huu, walinyanyua ufalme wa EPL msimu jana kwa alama 100. Kabla ya msimu huo, alama za juu zaidi zilizowahi kutwaliwa na Liverpool ni 86 walipoambulia nafasi ya pili mnamo 2009.
Kufikia sasa, ni wazi kwamba timu itakayomaliza kampeni za msimu huu katika nafasi ya pili itajivunia alama nyingi zaidi kuliko kikosi kingine chochote ambacho kimewahi kushikilia nafasi hiyo katika historia ya EPL.
Liverpool ambao watafunga kampeni za muhula huu dhidi ya Wolves wikendi ijayo, wanasaka taji lao la kwanza la EPL baada ya miaka 29.