• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
WAKILISHA: Atumia Hip hop kuongoa vijana

WAKILISHA: Atumia Hip hop kuongoa vijana

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA enzi ambapo muziki umegeuzwa na kuwa jukwaa la burudani pekee huku wanamuziki wengi wa kisasa wakishutumiwa kwa kupotosha vijana, yeye ameamua kutumia nyimbo anazotunga kuwafungua macho barobaro na kupitisha ujumbe wa matumaini hasa kwa wanaotoka familia maskini.

Ni kazi ambayo James Kimari, 26, ambaye anafahamika kwa wengi kwa jina Mizani Boss amekuwa akifanya kwa miaka kumi sasa.

Anaendesha shughuli hizi akiwa nchini Amerika ambapo pia anafanya kazi kama mtaalamu wa usingaji(massage therapist).

Kama mwanamuziki, Mizani Boss ambaye alihamia Amerika miaka mitano iliyopita, anatumia kipaji chake pia kama mwanaharakati kueneza ujumbe mkali.

“Muziki wangu unazungumzia matatizo ambayo mwananchi wa kawaida anapitia kila siku kama vile ufisadi, njaa, vita na hata mahusiano miongoni mwa masuala mengine yanayozidi kuathiri raia wa Afrika. Najiona kama kioo cha jamii au mwalimu wa maisha na hivyo jukumu langu ni kuhamasisha na kuelimisha jamii,” anaeleza Mizani Boss.

Kwa sasa ana zaidi ya vibao 21 ambavyo tayari viko katika majukwaa ya mtandaoni.

“Baadhi ya nyimbo zangu ni pamoja na Janga Kuu, kibao kinachozungumzia athari za ufisadi. Pia, kuna Vizaazaa, wimbo ambao unazungumzia pandashuka za mahusiano na ndoa. Kibao hivi pamoja na vingine 14 vyaweza kupatikana kwenye mtandao wa soundcloud,” anaongeza.

Uzito wa kazi zake umekuwa jukwaa la ushauri kwa vijana sio tu hapa Kenya alikozaliwa, bali pia eneo la Boston, Massachusetts anakoishi.

Mzawa wa eneo la Lower Kabete, Kaunti ya Kiambu, Kimari aliondoka nchini baada ya kukamilisha masomo yake ya shule ya upili.

“Nilihamia Amerika kwenda kusaka kipato, lakini hata baada ya kupata ajira kama mtaalamu wa usingaji, nilihisi kwamba singeacha kipaji changu cha uandishi na uimbaji kutokomea,” anaeleza.

Safari yake kimuziki ilianza akiwa angali mdogo ambapo tayari alikuwa akijihusisha na uandishi wa mashairi na makala.

“Nilianza kuwa na maono haya nikiwa mdogo. Ni ndoto ambayo hata hivyo ilianza kudhihirika nikiwa katika shule ya upili kwani ni hapa ndipo nilianza rasmi uandishi. Nilihisi kuwa mimi ni kama chombo cha kupitisha ujumbe wa busara kwa watu,” anasema.

Vibao

Hata hivyo, alijitosa rasmi katika sanaa miaka kumi iliyopita alipoanza kurekodi vibao vyake.

Uanaharakati na moyo wake wa kutaka kusaidia hauishii tu hapo kwani amekuwa akisaidia wasanii wa humu nchini na anakoishi.

Anafanya hivi kupitia vuguvugu aliloanzisha la Wale Wabaya Ministries ambalo amekuwa akiliongoza huku likitoa huduma ya unasihi kwa washairi na wachoraji nchini Kenya na Amerika.

“Takriban washairi na wachoraji 20 wamenufaika kutokana na mradi huu wa unasihi,” anaeleza.

Aidha, jukwaa hili limekuwa likisaidia wasanii wa humu nchini kuuza bidhaa zao katika soko la Amerika.

Kupitia mradi huu ananunua bidhaa mbalimbali za sanaa, huku pia akisaidia kufanyia mauzo muziki wa wasanii kutoka humu nchini.

“Kwa kawaida mimi hununua bidhaa hasa za mapambo kutoka masoko ya Maasai Market na Kariakor kisha nazipeleka Amerika na kuuzia wakazi. Mbali na kusaidia wanaounda bidhaa hizi kujitegemea kiuchumi, kununua bidhaa zao ni njia ya kuzipa mfichuo kwa soko jipya,” anaongeza.

Kwa sasa Mizani Boss anasema kwamba amejiandaa kutayarishia mashabiki wake muziki zaidi huku akitumai kushirikiana na wanamuziki wengine wenye mawazo sawa na yake.

You can share this post!

Watu 41 wafa katika ndege ya Urusi, 37 wakwepa kifo

ULIMBWENDE: Jinsi ya kuondoa weusi chini ya macho

adminleo