ANNE CHESEREM: Uvimbe huu uliolemea madaktari umefanya jamaa na marafiki kumtoroka
NA RICHARD MAOSI
ANNE Cheserem Saurei ni mama wa wavulana wawili katika Kaunti ya Nandi. Amepitia changamoto za kulea wanawe huku akiuguza uvimbe wa mdomo alioupata miaka 10 iliyopita.
Kufikia sasa hawezi kutekeleza mambo muhimu maishani kama vile kula, kunywa wala kuzungumza sawasawa kama alivyokuwa zamani.
Anasema mnamo 2009, wanawe wakiwa shule alianza kupata uvimbe kinywani kama kipele kidogo lakini ukaendelea kuenea huku akidhani ni maumivu ya meno.
Alichukua hatua ya kuzuru zahanati moja katika eneo la Nandi alipodungwa sindano lakini badala ya kupona uvimbe ukaongezeka.
Kupitia ufadhili wa majirani na michango ya harambee, alielekezwa katika hospitali ya Mosoriot Health Centre, lakini huko madaktari wakashindwa kumshughulikia wakisema uvimbe ulikuwa juu ya ulimi.
Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, anasema wakati huo mwili wake ulikuwa umedhoofika sana lakini katika zahanati ya Mosoriot, alipewa dawa ya kurejesha tu afya ya mwili.
Bali na hayo, alipatiwa dawa ya kuzima maumivu kisha akarejea nyumbani. Madaktari wa Mosoriot walimshauri atembelee Hospitali Kuu ya Kenyatta au Kisumu ambapo aliahidiwa kuwa angeshughulikiwa.
“Walinieleza hizo ni hospitali ambazo zimejistawisha kuanzia kwenye maabara na vipimo,wakanihakikishia kuwa ningesaidika, lakini huko pia hali ilishindikana,”alisema.
Bali na kanisa kumchangia ili akapate matibabu Kisumu, anaungama kuwa amechoka kuzuru vituo vya afya.
Madaktari katika Hospitali ya Oginga Odinga Kisumu, walimshauri kuanza kula lishe bora kwa wiki sita ili mwili urejeshe afya yake lakini Bi Ann alijua huo ulikuwa ni mzaha kama kawaida.
Kufikia sasa amekaribia kukata tamaa akisema ni kama hospitali zote zimeshindwa kumshughulikia.
Aidha anasema hajui ni maradhi gani haya, kwa sababu amekuwa akipokea habari tofauti kutoka kwa madaktari.
Uvimbe wake umemfanya kutengana na jamii na marafiki, wengi wao wakisema anawafilisisha kutokana na gharama kubwa za matibabu..
Mnamo 2012 alirejeshwa kwenye hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Eldoret na akafanyiwa uchunguzi wa kina, baadaye 2016 vipimo vilibainisha hakuwa akiugua maradhi ya saratani.
Anne anasema amebakia kutegemea miujiza na kumtegemea Mungu tu, akisema labda hospitali zote nchini zimekata tamaa naye.
Wanawe, Duncun Kiprono mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya upili ya Kisii, na Daniel Kiptoo, mwanafunzi wa ualimu katika Chuo Cha Kenyatta jijini Nairobi, wamekuwa wakitegemea misaada kutoka kwa jamaa na marafiki, kwa muda sasa.
Mola alimjalia Duncun ambaye ni mwerevu darasani kupata ufadhili wa benki ya Equity, almaarufu Wings to Fly.
Benki ya Equity iliona haja ya kuingilia kati na kufadhili masomo yake wakiamini kuwa Duncun alihitaji msaada wa dharura.
“Tunaamini kuwa mama yetu atapata msamaria mwema atakayegharamia matibabu yake ili arejelee hali yake ya kawaida,” Duncun alisema.
Kutokana na hali kwamba yeye ni mjane na hana kazi yoyote, wanawe hulazimika kufanya vibarua kukabiliana na hali ya umaskini unaowakodolea macho.