Kitambue kikosi cha Twomoc FC
NA RICHARD MAOSI
TWOMOC FC ni kikosi kilichoanza mnano 2005 kushiriki ligi ya daraja la pili katika Kaunti ya Nakuru.
Ni timu yenye maono na mafanikio mengi yasiyoweza kupigiwa mfano. Inawaleta pamoja vijana kutoka mitaa ya Kaptembwa, Lanet, Pipeline, Freearea na Kiamunyi.
Mkufunzi Knight Lugalia alianzisha mishemishe mashinani ili kusaka vipaji miongoni mwa vijana waliotaka kujiendeleza katika ulingo wa soka kwa siku za baadaye kama taaluma.
Pili alitaka kuziba pengo kubwa baina ya timu zilizokubuhu ligini, na wachezaji chipukizi wanaoinukia kwa madhumuni ya kusakata hatimaye.
Alieleza kuwa mechuano ya kirafiki pamoja na ile inayoandaliwa na shirikisho la FKF tawi la Magharibi imekuwa ikiwapatia vijana nguvu na motisha .
“Kuwakabili wapinzani bila woga kwa kutumia ujuzi wanaopata uwanjani wakati wa mazoezi ni jambo la kuwatia shime wachezaji wanaoibukia,” alisema.
Kikosi cha Twomoc FC kina jumla ya wachezaji 46 huku timu zikigawika kwa makundi matatu ya wachezaji 15 hivi ukiongeza na wale wa akiba,yaani U-10,U-15 na U-20.
Ikiwa timu iliyopeperusha bendera ya kaunti vizuri katika michuano takriban yote,vijana wengi wanatamani kujiunga nao.
Uwanja wao wa nyumbani unafahamika kama Kamukunji,ambapo kila siku za wiki wachezaji hujumuika kupasha misuli moto kuanzia 5.00 alasiri.
Twomoc ndiyo klabu yenye mashabiki wenye ufuasi wa dhati wengi wao wakionyesha mapenzi ya kweli kwa kushabikia kikosi kinaposhiriki michuano ya nyumbani.
Ni timu iliyoinua vipaji vya haiba ambavo baadae hutumika kwenye ligi ya KPL kama vile Aron Mwale wa Ulinzi Stars na mnyakaji hodari David Mwaniki aliyetamba katika shirikisho la michuano ya shule za upili 2018/2019.
Kutokana na kabumbu yake safi,ni fahari kubwa wanapokabana koo na watani wao wa jadi Community 08,mechi inayozua msisimko wa aina yake na kujaza uwanja.
Mkufunzi Lugalia anasema cha msingi ni bora mchezaji kuzingatia nidhamu ya hali ya juu,kuweka bidii na kushirikiana na wenzake.
Anasema kikosi chake kinajiamini na kila mara waingiapo uwanjani anafahamu fika kuwa anatumia zana mahiri.
Katika jumuia ya mashindano wameweka kibindoni mataji takriban yote ukianzia taji la ligi ya kaunti ya Nakuru,Inter -Estate,Governors league,Charity Cup na nyinginezo nyingi.
Aidha wameliza timu nyingi,hasa Asek FC 4-0,Community 08 5-3,Kijabe 3-0,Nakuru Youth 1-0 na hivi punde Kimathi FC 2-0.
Anawapatia ushauri wachezaji waliopo sokoni,kuwa makini wanapoingia mikataba na vilabu hivyo.Wasijiingize katika dili ambazo haziendani na vipaji vyao.
Wachezaji wajikaze katika juhudi za kujiboreshea mazingira ya kusakata kabumbu.
Lengo lao ni kupanda daraja na kushiriki ligi ya divisheni ya kwanza(supa) na baadae ligi ya Sportpesa.
Mkufunzi Knight anawashauri wazazi kuwaruhusu watoto wao kufuata ndoto zao huend wakaja kuwa watu wa maana kwenye ulimwengu wa soka..