Michezo

Kipsang’ kujaribu bahati Tokushima Marathon

March 4th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya kushindwa kumaliza mbio za Tokyo Marathon nchini Japan hapo Februari 26, Mkenya Wilson Kipsang’ ameamua kujaribu bahati nchini humo tena katika mbio za Tokushima Marathon mnamo Machi 25, 2018.

Kamati Andalizi ya Tokushima Marathon imetangaza kwamba Kipsang’ ni mmoja wa wakimbiaji 181 wa kigeni waliojiandisha kuwania taji. Jumla ya wakimbiaji 14, 200 wameingia makala haya.

Ili kuongeza ushindani, waandalizi wa mbio hizi, kwa mara ya kwanza kabisa, wamejumuisha Wakenya watatu. Kipsang’ anajivunia amekamilisha mbio hizi za kilomita 42 kwa muda wake bora wa saa 2:03:13 aliopata kwa kumaliza Berlin Marathon katika nafasi ya pili nchini Ujerumani mwaka 2016.

Alishinda Tokyo Marathon mwaka 2017 kwa saa 2:03:58, ambao ni muda mzuri kabisa kuwahi kuwekwa katika ardhi ya Japan. Rekodi ya Tokushima Marathon ni saa 2:15:25. Iliwekwa na Mjapani Yuki Kawauchi mwaka 2014.