Michezo

Matumaini tele kikosi cha riadha kitanogesha Japan

May 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

NAHODHA wa kikosi cha Kenya, Aaron Koech ni mwingi wa matumaini kwamba wataendeleza ubabe walioudhihirisha katika Riadha za Afrika mwaka 2018 watakapopeperusha bendera ya taifa jijini Yokohama, Japan wikendi hii.

Jiji la Yokohama litakuwa mwenyeji wa Mbio za Dunia za kupokezana vijiti kati ya Mei 11-12, 2019.

Koech amesema kwamba wako tayari kutamba zaidi katika kivumbi hicho na kufuzu kwa fani mbalimbali za mbio za masafa mafupi katika Riadha za Dunia zitakazoandaliwa jijini Doha, Qatar kati ya Septemba 28 na Oktoba 6, 2019.

“Tumejiandaa vya kutosha na tuko tayari kukabiliana vilivyo na wapinzani wetu na kuendeleza makali tuliyoyaonyesha jijini Asaba, Nigeria katika Riadha za bara la Afrika mwaka 2018,” akasema Koech ambaye pia alikuwa nahodha wa kikosi cha Kenya katika mbio hizo za Nigeria.

Kikubwa zaidi ambacho kinampa Koech tumaini kwamba kikosi cha Kenya kitanogesha vilivyo mbio za Japan mwishoni mwa wiki hii ni ukubwa wa kiwango cha mazoezi ambayo wanariadha wote walishiriki bila ya visa vyovyote vya majeraha kuripotiwa kambini.

“Makocha wametunoa vilivyo na kumwelekeza kila mwanariadha ipasavyo, hasa kuhusu namna ya kuanza mbio, kuimarisha kasi na kupokeza kijiti kwa njia mwafaka,” akasema Koech kabla ya kuwaongoza wenzake kuelekea jijini Yokohama hapo Jumatano.

Kikosi cha Kenya ambacho kitashiriki mbio hizo za Japan kinawajumuisha watimkaji 24 na maafisa tisa.

Timu hiyo imekuwa ikijifua katika uwanja wa Nyayo, Nairobi tangu Aprili 18, 2019.

Kenya iliwahi kushinda medali katika makala matatu yaliyopita ya mbio hizi katika vitengo vya mita 4×800 na mita 4×1500.
Kenya inakabiliwa na mtihani mgumu wa kujizolea nishani katika vitengo vya mita 4×200 (wanaume), 4×200 (wanawake), 4×400 (wanawake), 4×400 (wanaume kwa wanawake) na 2x2x400.

Mmoja mmoja

Kitengo hiki cha mwisho kinahusisha mkimbiaji mmoja mwanamume na mmoja wa kike kukimbia jumla ya mita 800 kwa kubadilishana kijiti kila baada ya mita 400.

Mataifa 47 yatashindana katika makala ya nne ya mbio hizi za Japan.

Amerika na Jamaica zilikamilisha makala matatu yaliyopita yaliyofanyika mnamo 2014, 2015 na 2017 katika nafasi ya kwanza na pili mtawalia.

Aaron Koech (kulia) afanya mazoezi na Kiprono Kosgey mnamo Januari 4, 2019, katika uwanja wa Eldoret Sports Club. Picha/ Jared Nyataya

Kujumuishwa kwa kikosi cha Kenya katika mbio za mita 4×400 katika kivumbi hicho cha kupokezana vijiti ni afueni tele kwa wanariadha na mashabiki wa humu nchini.

Kocha wa kikosi cha Kenya, Stephen Mwaniki amefichua kwamba hatua hiyo ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) itawapa akina wa dada wa Kenya fursa maridhawa zaidi ya kufanya vyema na hivyo kufuzu kwa Riadha za Dunia zitakazoandaliwa jijini Doha, Qatar baadaye mwaka 2019.