UFUGAJI NA ZARAA: Ufugaji nguruwe humpa riziki nzuri
WAKATI Michael Koome Mburugu ambaye ni mhasibu na pia wakili jijini Nairobi alinunua shamba eneo la Maili Nane, Kaunti ya Meru, hakudhania kwamba shamba hilo katika eneo kame lingemfaidi.
Kufikia mwaka 2013 shamba hilo ambalo amekuwa akilinunua kwa kulilipia polepole, lilikuwa lenye jumla ya ekari 22 ndipo akaamua kuanzisha mradi ambao mbali na kumnufaisha binafsi, liliifaa jamii nzima.
Akishirikiana na mkewe, Bi Jennifer Kago-Koome, walijitosa kwa kilimo-biashara cha kukuza vitunguu maanake zao hilo lilionekana kuwaletea faida wakulima wa eneo hilo.
Ni uamuzi alioujutia baadaye.
Baada ya misimu miwili ya ukuzaji wa vitunguu, kutokana na wakulima wengi kukuza zao hilo hilo, na kujaza soko, hali iliyoshusha bei yake, aliachana na kilimo chake.
“Kilo moja ya kitunguu ilikuwa Sh100 hapo awali lakini bei hiyo ilishuka sana, hivi kwamba ilikuwa hasara kukuza vitunguu,” alisema. Hapo alilazimika kugura uwekezaji huo.
Wawili hao walichukua hatua nyingine.
Mara hii, waliamua kuwafuga nguruwe kwani mbuzi na ng’ombe hawakuwa rahisi kufugwa maeneo kame.
Waling’amua kuwa kufuga nguruwe kuna faida nyingi na pamoja na soko tayari la nyama yake kwenye vichinjio.
Mnamo 2014, kutokana na akiba yake, Michael alinunua nguruwe 30 ambao alianza kuwafuga kwenye ekari tano za shamba ambalo awali alikuwa amepanda vitunguu.
Baadaye, aliongeza nguruwe 20 na kwa muda mfupi, walikuwa nguruwe 220.
Kwa sasa, kwenye ekari tano, wana vipande tisa ambavyo wamefuga wana wa nguruwe katika vyumba 26 kwa kila kipande huku kila chumba kikiwa na nguruwe 12.
Shamba hilo ambalo limesajiliwa kwa jina Daiichi Farm Ltd, lina jumla ya nguruwe 2,700 aina ya Duroc, Landrace na Large White. Kulingana nao, ni mbinu bora za kuwafuga wanyama hawa ndizo zilizowazolea sifa kochokocho huku wakirina mamilioni ya hela.
Kwa mfano, Daniel Simiyu anayewatunza nguruwe hawa amehitimu katika masomo ya utunzaji wa mifugo katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Wafanyikazi wengine pia ‘wametosha mboga’ kutokana na elimu yao.
Kampuni ya Daiichi imewaajiri wafanyakazi 32 wa kudumu huku vibarua wakialikwa wakati kazi imeongezeka. Bi Koome anasema kwamba hawa wafanyikazi wote wamepewa makazi humo.
Awali, wanandoa hawa walipoanza kuwafuga nguruwe, walikumbwa na changamoto si haba, hususan lishe ya wanyama.
“Tulipokuwa wageni kwenye mradi huu, tulikumbwa na vizingiti vya kununua lishe bora,” alisema Bw Mburugu.
Anasema kwamba walikuwa na wakati mgumu hivyo basi wakalazimika kujitengenezea lishe ili kupunguza gharama.
Waliomba msaada kutoka kwa mkulima wa kisasa kutoka Afrika Kusini ambaye aliwasaidia kusaga na kuchanganya lishe kutokana na viambato walivyokuwa wakitoa Nairobi.
Hivyo basi, wamekuwa wakitengeneza lishe kwa usaidizi wa mtaalamu wa mambo ya lishe, lishe ambayo huwafaa nguruwe wote, watoto na waliokomaa.
Wanapozaliwa, watoto wa nguruwe hunyonya kwa siku 10 kabla ya kuanza kupewa lishe maalum yenye viwango vya juu vya nguvu na virutubisho muhimu mwilini.
Kadri wakuavyo, nguruwe hao hupewa virutubisho vya kuwafaa kiumri.
“Sisi hutengeneza tani 6.5 ya lishe kila siku. Na nguruwe hula tani 4.5 kila siku,” anasema Simiyu ambaye ni mmoja wa wafanyakazi.
Anaeleza kwamba wao huwalisha nguruwe mara tatu kila siku – alfajiri, adhuhuri na jioni ambapo nguruwe wengi hula kilo tatu kila siku kinyume na nadharia ya wengi ambao hudhania hula sana.
Watoto hawa hupewa lishe kulingana na kiwango kwani ni vigumu kukadiria kiwango cha lishe wanayohitaji.
Wao huoshwa baada ya wiki moja. Simiyu anasema kwamba wao huwadunga dawa ili kuwasafisha, kazi anayosema si rahisi.
Maji huwekwa kwenye zizi na nguruwe huwa wamefunzwa kuyanywa maji kwenye videbe vilivyowekwa vyumbani.
Dkt Koseph Mugachia ambaye ni mwenyekiti wa Garden Veterinary Services Ltd anasema kwamba nguruwe hupewa lishe yenye virutubisho vingi na usafi wa hali ya juu.
Hii ni kwa sababu nyama ya nguruwe inafaa kuwa safi kuliwa hivyo inabidi mkulima afanye hima kuwakuza kwa mazingira ya usafi.
Kulingana na mtaalamu huyo, ugonjwa wa African Swine Fever (ASF) ni hatari sana kwani ugonjwa huo una uwezo wa kuwaua nguruwe wote walio kwenye shamba hili.
Chanjo
Anasema kwamba hakuna chanjo hadi sasa dhidi ya ugonjwa huu ambao huenea kwa kasi mno. Tatizo lingine lilikuwa kuwasafirisha nguruwe hawa hadi vichinjioni na sokoni.
Kulingana na Michael, awali, malori ya kuwasafirisha nguruwe hawa sokoni yalikuwa yakitozwa ushuru wa uchukuzi. Hata hivyo, alipata suluhu.
Maji pia yalikuwa tabu hapo awali kwa kuwa eneo hili ni kavu lakini walilazimika kuchimba bwawa la maji.
“Tumezingatia viwango vya hali ya juu ya utunzaji wa nguruwe hawa. Kuanzia kuzaliwa kwao, kuwang’oa watoto meno hadi kudhibiti kujamiiana kwao. Hatumruhusu yeyote kutembea kwenye shamba hili kiholelaholela,” anasema Bi Koome.
Wananguruwe pia huwekwa kwenye maeneo maalumu ili wakue haraka na kuzuia kuumia kwao wanapoumauma mikia.
Baada ya siku tatu, wananguruwe hudungwa sindano ya kirutubisho cha Iron.
Kulingana na Simiyu, kufanya hivi huwapa nguvu kwenye mifupa.
“Baada ya siku 21, wao huhasiwa (kukatwa nyeti) kwani ili kuongeza uzani wao na kuvutia wateja sokoni,” anasema.
Magonjwa ya virusi na bakteria pia ni changamoto nyingine ambayo huwakumba wafugaji kwani yana uwezo wa kuangamiza nguruwe wote kwa muda mfupi.
Kuligana na Michael, ufugaji wa nguruwe bado una visiki si haba. Anasema kwamba kuna ukosefu wa miundombinu mwafaka kuhusu ufugaji wa wanyama hawa.