Makala

Waelezea jinsi wanavyofurahia maendeleo Thika

May 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

THIKA imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa ajenda nne kuu za serikali hasa kutokana na ushirikiano mzuri uliopo.

Kamishna wa Kaunti ya Kiambu, Bw Wilson Wanyange, alizuru kaunti ndogo ya Thika mnamo Jumanne wiki hii ili kujionea mwenyewe baadhi ya maendeleo katika eneo hilo.

Afisa huyo aliandamana na Mbunge wa Thika Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina, ambapo walishuhudia maendeleo ya barabara na kilimo.

Bw Wanyange alizuru eneo la Umoja hadi Thika By-Pass ili kujionea barabara ya kilomita 10 itakayoendeshwa ujenzi wake na KURA ili kupunguza msongamano wa magari ya kuingia na kutoka mji wa Thika.

Wakati huo pia alizuru eneo la Komu ambako wengi wa wakazi hujishugulisha na kilimo.

Wakazi wa eneo hilo wanazingatia kilimo cha kunyunyizia mimea maji.

Nimeridhika na maendeleo yote niliyoshuhudia, na kwa hivyo nawahimiza wakazi wa eneo hii wazidi kujizatiti ili wanufaike na jasho lao,” alisema Bw Wanyange.

Bw Wainaina alisema lengo lake ni kuona ya kwamba ajenda nne muhimu za serikali zinazingatiwa.

“Tayari tumejionea barabara ambazo zimerekebishwa. Kuna ile inayopitia BAT ikielekea Delmonte By-Pass na kupitia shule ya Imani ikielekea Kang’oki hadi Munyu,” alisema Bw Wainaina.

Alisema barabara ya Thika-Kenol, itakarabatiwa upya kwa sababu ya magari mengi kuteleza eneo hilo mara mvua inyeshapo.

Alisema pia ile ya Blue-post itarekebishwa.

Alisema mradi wa maji wa Ndumago, uliogharimu Sh30 milioni umewafaidi wakazi wapatao 10,000 wanaoishi eneo la Magogoni na Ndula, Thika Mashariki.

Mhandisi

Mhandisi anayerekebisha barabara za mji wa Thika na vitongoji vyake Bi Jecinter Mwangi alisema kampuni ya Tosha Holding ndiyo inayokarabati barabara hiyo.

Alieleza mradi huo unastahili kuendeshwa kwa miezi michache na utagharimu takribani Sh26 milioni.

“Tunatarajia kurekebisha barabara ya kuelekea kampuni ya Bidco-General Kago na lile la Kenyatta Highway mjini Thika,” alisema Bi Mwangi.

Katika kijiji cha Magogoni, mkulima mashuhuri Bw Julius Kiiru, alionyesha jinsi ameweza kufanya kilimo biashara katika shamba la ekari moja na kufanikiwa.

Mkulima Bw Julius Kiiru Julia akielezea jinsi anavyoendesha kilimo chake katika shamba lake katika kijiji cha Magogoni, Thika Mashariki. Mbunge Patrick Wainaina (kati) akimpa sikio mkulima huyo. Picha/ Lawrence Ongaro

Mkulima huyo anaendelea kukuza matunda aina tofauti, malenge, mihogo, mapapai, na nyanya za kisasa.

“Mimi tangu nianze kilimo hiki kama miezi minane iliyopita nimeweza kufanikiwa pakubwa. Nimepata mazao ya kutosha na nimefaidika kulea familia yangu,” alisema Bw Kiiru.

Alipongeza juhudi za mbunge wake kwa kuhakikisha wanapata maji hapo mashinani ambapo yameweza kusaidia wakazi wengi wa eneo hilo.

Alisema vijana wengi sasa wamejitolea kuingilia kilimo kwa sababu maji yanapatikana kwa wingi sasa.

“Vijana sasa wanajiajiri wenyewe kwa kukuza nyanya, vitunguu na viazi ili kuweza kupata riziki badala ya kujihusisha na mambo maovu,” alisema Bw Kiiru.