Habari

Namtaka mzee wangu

May 11th, 2019 2 min read

Na ERIC WAINAINA

KESI ambapo wakili maarufu jijini Nairobi Assa Nyakundi alishtakiwa kwa kumpiga risasi na kumuua mwanawe, ilichukua mkondo mpya jana baada ya mkewe, ambaye awali alikuwa mmoja wa mashahidi wakuu, kubatilisha taarifa yake ya awali iliyomshutumu Bw Nyakundi na kuomba mumewe arudi nyumbani.

Kupitia kwa mawakili wake wanaoongozwa na Bw Shadrack Wambui na wale wa mshtakiwa wanaoongozwa na Bw John Khaminwa, Bi Lydia Nyakundi alisema amekubali hali ilivyo baada ya kifo cha mwanawe na sasa anataka kurudiana na mume wake.

Wiki mbili zilizopita, Nyakundi aliagizwa na mahakama asiende karibu na nyumba yake iliyoko mtaa wa kifahari wa Muthaiga.

Bi Lydia na mwanawe mkubwa, Bw Noah Nyakuru, walikuwa mashahidi katika kesi hiyo ambapo Bw Nyakundi ameshtakiwa kwa mauaji ya mwanawe, Bw Joseph Bogonko mnamo Machi 17 bila kukusudia.

Kulingana na Lydia, kifo cha mwana wao kilikuwa ajali. Anadai alithibitisha hayo kupitia kwa upelelezi wake wa kibinafsi uliomwezesha kutambua mume wake hana hatia kwa kuwa hakukusudia kumuua mwana wao.

Wakili Khaminwa alisema mshtakiwa, ambaye amekuwa akiishi katika nyumba ya kukodisha katika mtaa wa Kilimani baada ya kuagizwa na korti asiende nyumbani kwake, anastahili aruhusiwe “kuungana na mke wake mpendwa na watoto” kwani wamekubali kurudiana naye, na hilo ni jambo ambalo mahakama haiwezi kuzuia.

“Kile ambacho (upande wa mashtaka) mnamfanyia Nyakundi (kwa kumshtaki) ni dhuluma isiyoweza kukubalika. Hatuwezi kuporomosha familia jinsi hii. Tunaharibu familia ya Nyakundi. Mke wake anamtamani sana mumewe,” akasema.

“Hakuna mwanamke mwenye akili timamu, anayefahamu au aliye na ushahidi kwamba mume wake alihusika kwa mauaji ya mwanao angetaka kurudiana naye, kuishi pamoja kwa nyumba moja na kulala kitanda kimoja. Katika kesi hii, mwanamke husika anamtaka mume wake arudi nyumbani. Watoto wanataka baba yao arudi nyumbani,” Bw Khaminwa aliambia mahakama.

Ijumaa, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupitia kwa msaidizi wake, Bi Catherine Mwaniki, aliwasilisha ombi kwa Hakimu Mkuu wa Kiambu, Bi Terresia Nyangena akisema afisi hiyo haitaki tena kuendeleza mashtaka ya mauaji bila kukusudia kwani wakili Nyakundi anastahili kushtakiwa kwa mauaji.

Kuua bila kukusudia

Shtaka la mauaji liligeuzwa kuwa la mauaji bila kukusudia kwa vile hapakuwa na ushahidi wa kutosha, na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI), Bw George Kinoti anaamini hii ilitokana na utepetevu katika upelelezi uliofanywa.

Kutokana na jinsi mawakili wa upande wa mshtakiwa walivyoungana na wa Bi Lydia, upande wa mashtaka huenda ukakumbwa na changamoto zaidi katika kuendeleza mbele kesi hiyo.

Bi Mwaniki alisema inashtusha kwamba Bi Lydia anaonekana ghafla hataki haki itendeke kwa mauaji ya mwanawe na anaamini kuna nia fiche.

Kulingana naye, Bi Lydia ni shahidi ambaye tayari alikuwa ameandikisha taarifa kisheria na ni lazima atoe ushahidi kuhusu kifo cha mwanawe.

“Huyu ni mama ambaye alimbeba mtoto kwa miezi tisa tumboni. Mama yeyote angetaka kujua ni nini hasa kilitokea; kwa hivyo inafaa aruhusu DPP na DCI kutumia kila mbinu ili mtoto wake, Joseph Nyakundi atendewe haki,” akasema Bi Mwaniki. Kesi hiyo itaendelea Ijumaa wiki ijayo.