Ruto akosoa Raila kuhusu wito wa mageuzi ya Katiba
Na SAMMY LUTTA
NAIBU Rais William Ruto amekemea msimamo wa Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga kuhusu mageuzi ya Katiba.
Mnamo Ijumaa, Bw Odinga alijitokeza kwa kishindo na kutangaza kwamba, marekebisho ya katiba yatafanyika na yeyote atakayejaribu kuyazuia atajipata pabaya kwani atamezwa na mawimbi ya mabadiliko.
Hata hivyo, Jumamosi, Dkt Ruto alisisitiza hizo ni njama za hasimu wake wa kisiasa kujitakia makuu.
“Mabadiliko ambayo baadhi ya viongozi wamekuwa wakizungumzia yanalenga tu kuimarisha maisha ya wanasiasa fulani ili waendelee kuwa na mamlaka zaidi. Tunataka kuwaambia kuwa Kenya sio ya viongozi wa kisiasa pekee, taifa hili lina zaidi ya wananchi 45 milioni,” akasema Dkt Ruto.
Alitoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuangazia masuala ambayo yataimarisha maisha ya wananchi ambao waliwachagua.
“Kama serikali ya Jubilee, hatushughulikii masuala ya uchaguzi na ugavi wa vyeo wakati huu. Mabadiliko ambayo wananchi wanatarajia ni yale ambayo yataimarisha maisha yao,” akasema akiwa Lokichar, eneobunge la Turkana Kusini.
Huku akionekana kumrejelea Bw Odinga ambaye aliambia wananchi yeye ni mganga wa kutibu matatizo ya kitaifa, naibu rais alidai baadhi ya viongozi wameungama kuwa wao ni wachawi na nguvu hizo ndizo watategema kutatua matatizo ya taifa hili.
Wakati huo huo, alizidi kukashifu vikali jinsi vita dhidi ya ufisadi vinavyoendelezwa nchini akisema haviwezi kuendeshwa kwa kutegemea propaganda na madai ya uwongo, bali kwa misingi ya ushahidi thabiti utakaowasilishwa kortini.
“Watu wengine wanasema wao ndio wanapambana na ufisadi nchini. Kuna tofauti kubwa kati ya kupambana na ufisadi na propaganda kuhusu ufisadi ambazo zinaendelezwa na matapeli fulani wa kisiasa ambao lengo lao ni kujitakia makuu wala sio kupambana na uovu huu,” Dkt Ruto akasema akionekana bado anamlenga Bw Odinga.
Ushahidi
Dkt Ruto alisema ikiwa mtu amejitolea kupambana na ufisadi, jambo la busara ni kwa mtu kama huyo kuwasilisha ushahidi kortini wala sio kupeleka vita hivyo katika hafla za mazishi na mikutano ya hadhara.
“Watu kama hao watafute watu wa kudanganya lakini sio Wakenya. Wajue kuwa kuna uhaba mkubwa wa wajinga nchini Kenya,” akasema.
Katika mikutano ya hadhara, Bw Odinga amekuwa akikariri kujitolea kwake katika vita dhidi ya ufisadi akisema ni mojawapo ya malengo anayotazamia kufanikisha kupitia ushirikiano wake na Rais Uhuru Kenyatta.
Tofauti na msimamo wa Dkt Ruto, Kiongozi wa Chama cha Amani National Congress, Bw Musalia Mudavadi jana alisema mienendo ya siku hizi ya Bw Odinga huenda ikafanya vita dhidi ya ufisadi visifanikiwe.
Akiwa katika eneobunge la Gem alipohudhuria harambee katika Shule ya Upili ya Sirembe, Bw Mudavadi alisema sakata za ufisadi zimezidi nchini na Bw Odinga asipojitokeza kwa ukakamavu, huenda taifa likaporomoka.
Viongozi wa Kanisa Katoliki walikuwa wameelezea wasiwasi wao Ijumaa kwamba, vita dhidi ya ufisadi vimeingia baridi ikizingatiwa kuwa kesi zilizoanzishwa zinaonekana kugonga mwamba mahakamani.