Western Bulls na Kisumu warejea 'meza ya wanaume'
Na GEOFFREY ANENE
WANARAGA wa Western Bulls na Kisumu wamerejea katika Ligi Kuu baada ya kunyakua tiketi kwa kushinda mechi za nusu-fainali za Ligi ya Daraja ya Pili, Jumamosi.
Bulls kutoka Kaunti ya Kakamega, ambayo ilitemwa 2016-2017, imechabanga Chuo Kikuu cha USIU kutoka Nairobi kwa alama 22-16.
USIU, ambayo pia iliwahi kushiriki Ligi Kuu miaka 11 iliyopita, iliongoza 6-0 kabla ya Bulls kupata mguso na mkwaju na kuongoza 7-6 wakati wa mapumziko. Bulls iliimarisha uongozi wake kipindi cha pili kilipoanza hadi 17-6.
Hata hivyo, USIU ilirejea dakika za mwisho na kupunguza mwanya huu hadi alama moja 17-16 kabla ya Bulls kujiwekea nafasi ya kupumua kupitia mguso kutoka kwa Miller Oroto.
Kisumu kutoka Kaunti ya Kisumu, ambayo ilishiriki Ligi Kuu mara ya mwisho msimu 2013-2014, ilirejea baada ya kuzima timu nyingine ya zamani wa Ligi Kuu, Catholic Monks kwa alama 14-11 katika muda wa nyongeza baada ule wa kawaida kumalizika 11-11.
Monks ilitemwa kutoka Ligi Kuu mwisho wa msimu 2014-2015.
Bulls na Kisumu zinachukua nafasi za Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi na Leos ya Chuo Kikuu cha Strathmore zilizoshushwa ngazi baada ya kumaliza msimu huu wa 2018-2019 katika nafasi mbili za mwisho.