• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
RAMADHAN: Tusiwasahau wasiojiweza katika mwezi huu wa kuliwazana

RAMADHAN: Tusiwasahau wasiojiweza katika mwezi huu wa kuliwazana

NA KHAMIS MOHAMED

Hakika mwezi wa Ramadhani ni msimu wa kufanya kheri. Ni mwezi ambao Waumini huonyesha aina zote za kheri. Hutumia mikusanyiko yao kuonyeshana undugu, ujamaa na huruma. Huonyesha upendo na ukarimu kwa majirani, wapita njia na kila mtu katika jamii bila kujifaharisha kwa mwingine.

Miongoni mwa kheri ni kutoa sadaka, kusaidiana na kuwa ma huruma haswa katika mwezi huu wa baraka. Kuwa na hima ya kuwasaidia wasiojiweza katika mujtamaa wetu kwa kuwafuturisha.

Mwenyezi Mungu amesema katika kitabu chake kitukufu “Saidianeni katika Kheri wala msisaidiane katika uovu.”

Sadaka ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ni bora kuliko sadaka katika miezi ya kawaida. Na ndio maana mtume (S.A.W) akauita mwezi huu ya kwamba ni mwezi wa kuliwazana.

Kwani masikini pia katika funga zao hupatwa na njaa na kiu, na mikononi mwao hawana kile kitakacho watosheleza, basi pindi wanapo patikana watu wanao wapatia sadaka na kuwafanyia ukarimu, nao hufarijika na kuliwazika.

kukirimiana ndilo jambo la kuleta furaha zaidi. Kule kuhisi kuwa mwenzangu amefunga kama mimi, na anafuturu kilekile ninachofuturu mimi kwenyewe tu kunaleta raha moyoni.

Na katika sadaka zinazotiliwa mkazo katika mwezi wa Ramadhani ni kuwafuturisha waliofunga, amesema Mtume (s.a.w): Mwenye kumfutarisha aliyefunga anakuwa na malipo mfano wa malipo ya aliyemfutarisha na hayapungui malipo ya aliyefunga kitu chochote.

Kwa kuzingatia Hadith hiyo, hebu mtu apige hesabu ya fadhila atakazozipata kwa kila kichwa cha mfungaji anayemfuturisha. Hapana shaka hii ni fursa ya kipekee ya kupata fadhila nyingi za Mwenyezi Mungu kwa wakati mmoja.

Anasema mtume (S.A.W) “Yule mwenye kumfuturisha mfungaji katika mwezi huu wa Ramadhani basi kitendo chake hicho kitakuwa ni kafara ya madhambi yake. Na ataachwa huru na moto wa jahannam. Na atakuwa na malipo mfano wa malipo ya mfungaji, pasi na ya kupungua malipo ya mfungaji japo kidogo”

Hadithi hizi ni dalili tosha kuonesha ubora wa sadaka ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Ukarimu katika mwezi huu wa ramadhani hauishii katika kutoa sadaka tu, bali ikiwezekana hata kuwakusanya masikini na kufuturu nao pamoja. Shughuli hii licha ya kupata thawabu kwa mfangaji lakini huwa ni yenye kumuondolea mja kiburi na kujiona katika moyo wake

Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni msimu wa utiifu wa hali ya juu, ukarimu, sadaka na kheri mbali mbali. Na wala si mwezi wa ubakhili.

You can share this post!

Wanafunzi 2 wafa shuleni katika hali tatanishi

Wakazi wa Matungu waamua kuua washukiwa wa mauaji

adminleo